Mfanyabiashara James Rugemalira, ametoa notisi kwa taasisi tisa, ikiwemo Usalama wa Taifa, TAKUKURU, Gavana wa Benki Kuu, DCI, TRA, Wakili Mkuu wa Serikali, Kamishna wa Magereza pamoja na kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini akiomba amtoe kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili.
Rugemalira ameyabainisha hayo leo February 13, 2020 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipofikishwa kwa ajili ya kutajwa na kusema kuwa asipofanya hivyo atawasilisha hoja rasmi za kuondolewa katika kesi hiyo Mahakamani ambapo upande wa mashtaka kupitia kwa Wakili wa Serikali Wankyo Simon alisema kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Baada ya Wakili Wankyo kusema hivyo Rugemalira alinyoosha mkono akiomba kuzungumza na aliporuhusiwa alidai kuwa notisi alizoziandika na kuzituma zote zimepokelewa sehemu husika na hivyo alitarajiwa leo kuachiwa na kuondolewa katika shauri hilo.
“Nilitegemea leo Jamhuri waje na ufafanuzi juu ya barua niliyoandika kuhusu Benki ya Standard Chartered kukwepa kodi, sheria haitekelezwi, jana nimetoa notisi na kuisambaza na imepokelewa kote,” Rugemarila.
Rugemalira pamoja na mmiliki mwenza wa zamani wa kampuni ya IPTL, Harbinder Sethi, wanakabiliwa na mashtaka 12 ikiwemo utakatishaji wa fedha, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, utakatishaji wa fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27 za Tanzania, makosa ambayo wanadaiwa kuyatenda jijini Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.
Social Plugin