Serikali za Uganda na Rwanda, Jumapili zilikubaliana kubadilishana wafungwa, katika juhudi za kupunguza uhasama baina yao, baada ya kushutumiana kwa mda mrefu na kufanyiana ujasusi unaotajwa na wachambuzi kama wenye lengo la kutatiza amani ya kila upande.
Rais wa Rwanda Paul Kagame, na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni ambao walikuwa marafiki wakubwa sana kabla ya kutofautiana, walifikia makubaliano hayo katika kikao cha mjini Luanda, Angola.
Viongozi hao hao walisaini mkataba wa ushirikiano katika kurejesha hali ya utulivu baina yao, mwezi Agosti mwaka uliopita, lakini utekelezaji wake umekosa kasi ilivyiotarajiwa.
Japo hakuna taarifa zaidi zimetolewa kuhusu makubaliano ya jumapili, inafahamika kwamba viongozi hao wawili walikubaliana kubadilishana wafungwa katika kikao kitakachofanyika Februari 21, kwenye mpaka uliofungwa kati ya Rwanda na Uganda, mjini Katuna .
Kikao cha Angola kilisimamiwa na rais Joao Lourenco, na kuhudhuriwa na rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi.
Katika taarifa ya kurasa mbili yenye vipengele 8 iliyotolewa na ikulu ya rais wa Angola, viongozi hao waliahidi kushirikiana katika kuimarisha amani, utulivu, ujirani mwema na kuaminiana.
“Pande zote mbili zinatakiwa kujizuia na vitendo vinavyoweza kuleta hali ya kutoaminiana au uhasama, kuhusiana na madai ya kufadhili makundi yenye lengo la kutatiza serikali zake,” kinasema kipengele cha pili, aya ya saba ya taarifa hiyo fupi.
Wiki iliyopita, rais wa Rwanda Paul Kagame alisema kwamba hatashurutishwa kufungua mpaka kati ya Rwanda na Uganda hadi serikali ya rais Yoweri Museveni itakapotimiza matakwa ya serikali ya Rwanda ambayo ni pamoja na kuachilia huru raia wake wote wanaozuiliwa katika magereza ya Uganda.
Rwanda ilifunga mpaka wake mwezi Februari mwaka uliopita na kupiga marufuku biashara kati yake na Uganda.
Hakuna taarifa iliyotolewa iwapo Rwanda ipo tayari kufungua mpaka wa Katuna ili kuruhusu raia wake kuingia Uganda, au Kuruhsu bidhaa za Uganda kuingia Rwanda.
Rwanda inaishutumu Uganda kwa kufadhili makundi ya waasi yenye lengo la kupindua serikali ya rais Paul Kagame.
-VOA