Mbunge wa kuteuliwa na Mhe. Rais ambaye ni Mke wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Mhe. Mama Salma Kikwete amekabidhi mabati 500 kwa ajili ya waathirika wa mafuriko, mabati 200 ujenzi wa Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi Halmashauri ya Mtama na mabati 60 ujenzi wa Shule ya Sekondari kata ya Mnara mkoani Lindi.
Akizungumza leo Jumatano Februari 26, 2020 wakati wa kukabidhi mabati hayo 760 Mama Salma Kikwete alisema : "Nimetoa mabati haya kwa kuwa mpaka sasa CCM haina Ofisi na wenzetu waathirika wa mafuriko wamepewa maeneo lakini bado wanahitaji msaada mkubwa katika kuhakikisha wanapata huduma pamoja na sehemu ya kuishi".
"Nipo tayari kusaidia waathirika wa mafuriko kwa chochote kama nilivyojitoa kuwapa mabati haya lakini nawaomba sana Watanzania kuendelea kuwasaidia waathirika waliopo Mchinga, Kilwa na maeneo mengine ambayo bado wananchi wetu hawajapa sehemu muhimu ya kuishi",amesema.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Rukia Hassan amempongeza Mh Mama Salma Kikwete kwa kutoa mabati 200 kwa ajili ya Ujenzi wa Ofisi katika Halmashauri ya Mtama.