Serikali ya Saudi Arabia imezuia wageni wote wanaoingia nchini humo kwa safari za kidini, ikiwemo wanaotembelea miji mitakatifu katika dini ya Kiislamu - Makka na Madina.
Mamilioni ya watu huingia Saudia mwaka mzima kufanya ibada ya Umra, na wengi zaidi huingia kwa pamoja kufanya ibada ya Hija.
Tofauti na Hija, Umra hufanyika katika kipindi chochote cha mwaka, na kwa sasa marufuku hiyo inawalenga mahujaji raia wa nchi za nje wanaoenda kuitekeleza.
Bado haijulikani kama ibada ya Hija, ambayo inategemewa kuanza mwishoni mwa mwezi Julai kama itaathirika na zuio hilo pamoja na kusambaa kwa virusi vya corona duniani.
Saudia pia imewapiga marufuku watu kutoka nchi zilizokumbwa na virusi hivyo kuingia nchini humo.
Mpaka sasa Saudia bado haina mtu ambaye amethibitika kuambukizwa virusi hivyo.
Makka, ndio mji ambao Mtume Muhammad alipozaliwa, na kuna msikiti mtakatifu zaidi. Madina ndipo alipofariki na kuzikwa.
Wizara ya mambo ya nje ya Saudia inasema marufuku hiyo ni ya muda - lakini wizara hiyo haijataja lini marufuku hiyo itaondolewa.
Watalii ambao si wa kidini ambao wanatoka katika nchi ambazo virusi vya corona vimethibitisha kuingia pia watakataliwa kuingia Saudia.