Serikaki ya Tanzania imewahakikishia wajumbe 11 wa kamati teule ya Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza kwamba wanaitambua Kampuni ya Mbogo Kampuni ya Mbogo Mining & General Supply Ltd na shughuli zote inazofanya nchini ni halali.
Kauli hiyo imetolewa na baadhi ya mawaziri akiwamo Waziri wa Madini, Doto Biteko , Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro katika vikao vilivyofanyika kwa nyakati tofauti na wajumbe hao.
Rais Nkurunzinza aliteua kamati hiyo kuja Tanzania na kukutana na viongozi wa Serikali ili kupata taarifa sahihi na uhalali wa kampuni hiyo ambayo inatarajiwa kukabidhiwa jukumu la kusambaza vilipuzi nchini Burundi sambamba na kushiriki mkutano wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini.
Akizungumza na wajumbe hao, Biteko alisema Serikali ya Tanzania haina shaka na kampuni hiyo na haijawahi kukiuka au kwenda kinyume na vibali vinavyotolewa na wizara, hivyo aliwataka kuondoa wasiwasi na kuipatia kazi nchini Burundi.
“Tunashukuru kwa ujio wenu maana shughuli ambazo zinafanywa na kampuni hii ni nyeti na zinaweza kuhatarisha usalama wan chi, lakini niwahakikishie kwamba tunafahamu kila kitu juu ya Mbogo Mining kwanza haijawahi kuleta shida tangu tunaipa vibali.
“Hapa nimeambatana na watalaamu ambao kila siku wanafanya nao kazi hivyo nawapa uhuru wa kuhoji kila kitu mnachotaka na majibu yatapatikana,” alisema
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda , Manyanya ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Riziki Shamdoe na watalaamu wengine alisema hawana wasiwasi na kampuni hiyo na inafahamika serikalini na wanashirikiana katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.
“Mbogo Mining imeweka historia hapa nchini kwa namna inavyowekeza na hadi nje ya nchi, kitendo cha kufika kwenu Burundi kimetuunganisha zaidi katika sekta ya viwanda na biashara na shughuli hii bila shaka itaongeza ajira kwa mataifa haya mawili,” alisema
Social Plugin