SERIKALI YAJIPANGA KUTOKOMEZA MAGONJWA YA MIFUGO NCHINI

Na. Edward Kondela

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema serikali itahakikisha inaendelea kutoa dawa za ruzuku za kuogeshea mifugo nchini ikiwa na lengo la kutokomeza kabisa magonjwa ya mifugo.

Naibu Waziri Ulega amesema hayo (22.02.2020) wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika mnada wa mifugo wa Ndelema uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Handeni Mkoani Tanga ambapo amewataka wafugaji kutoacha kuosha mifugo yao kwani kwa kufanya hivyo mifugo itakuwa na afya njema na hatimaye kupata bei nzuri ya soko.

“Mwaka jana tulipata pesa kutoka kwa mheshimiwa rais zaidi ya Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya kununua dawa na kugawa kwa majosho 1,400 nchi nzima, mwaka huu wametuongeza tumepata zaidi ya Shilingi Milioni 400 kwa ajili ya kununua dawa na kusambaza katika majosho 1,700 tutaendelea na zoezi hilo la kutoa dawa za ruzuku bila kuacha ili kuhakikisha tunapiga kabisa vita magonjwa ya mifugo.” Amesema Mhe. Ulega

Aidha kuhusu wafugaji wa Wilaya ya Handeni kuingiza mifugo yao katika misitu ya serikali Naibu Waziri Ulega akizungumza moja kwa moja kwa njia ya simu katika mkutano huo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo amemtaka kuweka alama katika misitu hiyo ili wafugaji waweze kutambua misitu ya serikali na kutoingiza mifugo yao kwa bila kukusudia.

Prof. Silayo amemuahidi Naibu Waziri Ulega katika mkutano huo kuwa atawatuma wataalamu siku ya Jumatatu ili kuanza utekelezaji huo mara moja na kuondoa migogoro ya wafugaji kuingiza mifugo yao katika misitu ya serikali.

Katika mkutano huo pia naibu waziri huyo ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni kuhakikisha unatua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo ikiwemo ya miundombinu katika mnada huo pamoja na barabara ili waweze kusafirisha mifugo yao kwa urahisi zaidi.

Nao baadhi ya wafugaji waliopatiwa nafasi kuuliza maswali na kutoa maoni yao juu ya sekta ya mifugo, wameipongeza serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikihakikisha inawaboreshea mazingira ya shughuli zao huku wakiomba wazidi kupatiwa elimu zaidi ya masuala mbalimbali ili wafanye shughuli zao bila kukiuka sheria za nchi.

Awali akitembelea bwawa la asili katika Kijiji cha Kweingoma kilichopo Wilaya ya Handeni Vijijini Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amewataka wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi katika bwawa hilo lenye urefu wa Kilometa Nne kujiunga katika ushirika ili serikali iweze kuwasaidia katika maeneo mbalimbali huku akiahidi kutoa mashine kwa ajili ya mtumbwi utakaotengenezwa na uongozi wa wilaya hiyo ili kurahisisha shughuli za uvuvi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amemaliza ziara ya kikazi ya siku tatu Mkoani Tanga ambapo amepita pia katika Wilaya za Muheza, Pangani, Mkinga na Halmashauri ya Jiji la Tanga na kuzungumza na wafugaji na wavuvi ili kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post