Somalia imekuwa nchi ya kwanza ya Pembe ya Afrika kutangaza kuwa, wimbi la nzige waliovamia nchi hiyo ni janga na kwamba kupambana na janga hilo ni jambo la dharura kitaifa.
Wizara ya Kilimo ya Somalia ilisema jana (Jumapili) kwamba wimbi kubwa la nzige waliovamia maeneo ya jangwani ni hatari kubwa kwa nchi hiyo ambayo tayari ina mazingira mabaya ya usalama wa chakula.
Taarifa ya wizara hiyo imeongeza kuwa, chakula cha wanadamu na mifugo yao kiko hatarini Somalia. Wimbi la nzige walioivamia nchi hiyo ni kubwa na wanaangamiza kiwango kikubwa cha mazao, mimea na majani.
Wizara hiyo imesema, tahadhari ya taifa iliyotangazwa na wizara hiyo inalenga kuhamasisha juhudi zaidi za kupambana na janga hilo na kuomba mataifa kuisaidia Somalia kwani kuvamiwa na nzige wakati huu wa kabla ya mwezi Aprili ambacho ni kipindi cha mavuno ni jambo hatari sana.
Nzige ni jamii ya panzi na wanapovamia shamba huangamiza kila kitu na kusababisha kutokea janga la njaa.
Waziri wa Kilimo wa Somalia, Said Hussein Iid amesema kuwa, kama hatua hazitachukuliwa hivi sasa, basi nchi hiyo itakumbwa na upungufu mkubwa wa chakula ambao itashindwa kukabiliana nao. Amesema, wametoa tahadhari hiyo kama njia ya kulinda usalama wa chakula kwa wananchi wa Somalia.
Social Plugin