Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SIMBA SC YAPUNGUZWA KASI LIGI KUU..... YACHAPWA 1-0 NA JKT TANZANIA



MABINGWA watetezi, Simba SC wamepunguzwa kasi baada ya kuchapwa 1-0 na JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam. 

Kwa kipigo hicho, JKT Tanzania inayofundishwa na kocha bora wa Ligi Kuu msimu wa 2017-2018, Abdallah Mohammed ‘Baresi’, inafikisha pointi 30 baada ya kucheza mechi 20, ingawa inabaki nafasi ya nne.

Kwa Simba SC Simba SC iliyo chini ya kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandonbroeck anayesaidiwa na mzalendo, Suleiman Matola, kocha wa makipa Muharami Mohamed ‘Shilton’ na kocha wa Fiziki, Mtunisia, Adel Zrane inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 50 za mechi 20 sasa, ikiwazidi pointi 12 Azam FC wanaofuatia.

Kiungo mpya wa Simba SC, Luis Miquissone akiwatoka wachezaji wa JKT Tanzania leo Uwanja wa Uhuru

Bao lililizamisha Simba SC leo limefungwa na nyota tegemeo la mabao la JKT Tanzania, Adam Adam kwa kichwa dakika ya 24 akimalizia krosi ya beki Damas Makwaya.

JKT Tanzania walicheza kwa nidhamu kubwa leo, wakiwabana wachezaji wa Simba na kuwatibulia mipango yao yote.

Dakika ya 51 mshika kibendera namba mbili Kassim Mpaga wa Dar es Salaam alimnyooshea kibendera cha kuotea kiungo Mbrazil wa Simba, Gerson Fraga ‘Viera’ wakati anamalizia kwa kichwa mpira wa juu wa kiungo Mkenya, Francis Kahata, ingawa hakuwa amezidi. 

JKT Tanzania walipata pigo dakika ya 77 baada ya kipa wao, Patrick Muntary kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Abdulrahman Mohamed ‘Wawesha’ aliyekwenda kumalizia vizuri.

Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Benno Kakolanya, Haruna Shamte, Gardiel Michael, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Gerson Fraga ‘Viera’/Clotous Chama dk63, Luis Miquissone, Jonas Mkude, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu/John Bocco dk63 na Shiza Kichuya/Fransis Kahata dk46.

JKT Tanzania; Patrick Muntary/Abdulrahman Mohamed dk78, Michael Aidan, Edward Songo, Edson Katanga, Damas Makwaya, Nurdn Mohamed, Mwinyi Kazimoto, Hafidh Mussa/Kelvin Nashon dk62, Mgandila Shaaban, Daniel Lyanga/Mussa Said dk90 na Adam Adam.
CHANZO- BINZUBEIRY BLOG

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com