Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke alipokutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam Februari 5, 2020.
Rais John Magufuli amemkabidhi barua Balozi wa China nchini Wang Ke aliyomwandikia Rais Xi Jinping wa nchi hiyo akimpa pole kwa janga la virusi vya Corona lililolikumba jiji la Wuhan na kusababisha vifo vya mamia ya watu.
Pamoja na kumkabidhi barua hiyo Balozi Wang Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania imeguswa na kulipuka kwa janga hilo na ipo tayari kutoa ushirikiano wowote ambao Serikali ya China itahitaji katika jitihada za kukabiliana na virusi hivyo.
“China ni ndugu zetu, ni marafiki zetu, tunatoa pole kwa Rais Xi Jinping na Wachina wote waliopatwa na madhara ya homa hii, daima Tanzania tupo pamoja na China na katika hili tupo pamoja pia” amesisitiza Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Balozi Wang Ke amemshukuru Rais Magufuli kwa kuguswa na janga hilo na kuungana na China katika kipindi hiki kigumu.
Ametumia mazungumzo hayo kueleza kuwa kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, China imeanza kupata mafanikio katika kukabiliana na Virusi vya Corona kwa kuzuia isienee katika nchi zingine.
Amemuhakikishia Rais Magufuli kuwa licha ya Tanzania kutokuwa na mtu yeyote aliyethibitika kuambukizwa virusi vya Corona, pia Watanzania 400 waliopo katika jiji la Wuhan ambao wengi wao ni Wanafunzi hawajaambukizwa na jitihada za kuhakikisha wanakuwa salama zinafanyika.