Serikali ya Marekani imepiga marufuku raia wa Tanzania kushiriki katika bahati nasibu wa kupata viza ya kuingia Marekani.
Bahati nasibu hiyo hutoa viza kwa watu takribani 50,000 kutoka nchi zenye kasi ndogo ya maendeleo kila mwaka kuingia na kufanya kazi Marekani.
Nchi ya Sudani pia raia wake wamepigwa marufuku kuingia katika bahati nasibu hiyo.
Wakati huo huo raia wa nchi nne ikiwemo mbili za Afrika Nigeria na Eritrea wamepigwa marufuku kabisa kuomba viza za kuhamia Marekani.
Hata hivyo raia wa nchi hizo ambao watataka kuingia Marekani kwa kutalii ama biashara wataruhusiwa.
Wiki iliyopita, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti juu ya rasimu ya marufuku mpya ya kuingia Marekani kwa mataifa saba.
Ni taifa moja tu la Belarus ambalo lilitajwa katika rasimu ya awali ambalo halijaorodheshwa katika taarifa za leo.
Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) limeripoti kuwa ofisa wa ngazi ya juu nchini Marekani amesema kuwa nchi hizo sita zimeshindwa kufikia kiwango stahiki cha ulinzi na kupashana taarifa.
"Nchi hizi kwa sehemu kubwa zinataka kutoa msaada lakini kwa sababu mbalimbali zimefeli kufikia viwango vya chini tulivyoviweka," amesema Naibu Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Chad Wolf.
Wolf amesema maofisa wa Marekani watakuwa tayari kushirikiana na nchi hizo sita ili kuimarisha matakwa ya ulinzi kwa nchi hizo ili iwasaidie kutoka kwenye orodha hiyo.
Social Plugin