Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
SERIKALI ya Tanzania imeweka wazi mipango na mikakati yake ya ufanikishaji wa malengo ya makubaliano ya kukuza uzalishaji, kujenga miundombinu na usambazaji wa nishati katika Nchi 15 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yaliyofikiwa na Viongozi Wakuu wa Kitaifa na Mawaziri wa sekta ya Nishati katika Jumuiya hiyo Mwezi Agosti mwaka 2019.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa wataalamu wa nishati kutoka Nchi za SADC unaoendelea Jijini Dar es Salaam leo Jumanne (Februari 25, 2020), Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said alisema mkutano huo unalenga kuanisha vyanzo na miradi mbalimbali ya kimkakati itakayowezesha utoshelevu wa nishati katika nchi za SADC.
Mhandisi Zena alisema kupitia Mkutano wataalamu wa sekta ya nishati wa Tanzania wataweza kubainisha fursa zilizopo katika kuhakikisha utoshelevu wa sekta ya nishati nchini ikiwemo Ujenzi wa Mradi Bwawa la kuzalisha Umeme kwa Kutumia maporomoko ya maji ya Bonde la Mto Rufiji wa Julius Nyerere (JNHPP) unaotarajia kuzalisha unaotarajia kuzalisha Megawati 2115.
‘’Tumeshuhudia majanga mbalimbali yanayotokana na mabadiliko ya baia nchi, sasa wataalamu wetu wa masuala ya nishati, mafuta na gesi watakutana na kujadili kwa pamoja ili kupata njia bora zaidi za kuweza kuzalisha nishati ya umeme itakayoweza kuwasaidia wananchi wetu’’ alisema Mhandisi Zena.
Alisema mipango na mikakati ya kuimarisha sekta ya nishati katika ukanda wa SADC ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Viongozi wa Kitaifa na Mawaziri wa sekta ya nishati katika Jumuiya ya SADC na Tanzania imepanga kuutumia vyema mkutano huo ili kuhakikisha kuwa sekta ya nishati inakuwa ya kibiashara na hivyo kuweza kutengeneza fursa kwa Watanzania.
Kwa mujibu wa Mhandisi Zena alisema mkutano huo wa wataalamu unatarajia kuhitimishwa mwishoni mwa wiki hii, ambapo mwezi Mei mwaka huu kunatarajia kufanyika Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa sekta ya nishati katika Nchi wanachama wa Jumuiya ya SADC, ili kuona namna bora zaidi ya utekelezaji wa miradi hiyo ili iweze kuleta tija na maendeleo endelevu kwa wananchi wa ukanda wa SADC.
Aliongeza kuwa mbali na miradi hiyo ya kimkakati, wataalamu hao hao pia watajadili fursa za nishati jadidifu na namna zinavyoweza kuongeza uwezo wa upatikanaji wa nishati ya umeme ili kuwawezesha wananchi wa ukanda wa SADC kuweza kuwa na nishati ya uhakika na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa yanayochangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Kamishna wa Nishati na Gesi kutoka Wizara ya Nishati, Adam Zuberi alisema mkutano huo umeshirisha jumla ya nchi wanachama 12 wa Jumuiya hiyo, ambao wanaandaa maazimio mbalimbali yanayotarajiwa kujadiliwa katika Baraza la Mawaziri wa sekta ya Nishati wa Jumuiya hiyo mwezi Mei mwaka huu.
Aliongeza kuwa katika mkutano huo, wataalamu hao pia watapata fursa ya kushiriki semina zitakazohusisha uwasilishaji wa mada na makongamano mbalimbali ya wadau wa sekta ya nishati ndani ya ukanda wa SADC.
Social Plugin