Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

USAJILI WADAU MNYORORO WA THAMANI WAJA

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Serikali imetangaza kuanza usajili wa wadau wote katika mnyororo mzima wa uongezaji thamani ya mazao ya kilimo.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma leo tarehe 6 Februari 2020, Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa Lengo la usajili huo ni kutaka kuwa na takwimu sahihi ya wadau mbalimbali wanaotoa huduma katika sekta ya kilimo nchini.

Ametaja wadau hao kuwa ni pamoaj na wakulima, watoa huduma mbalimbali za pembejeo, wasindikaji, wafanyabiashara za mazao, Taasisi za fedha, watoa huduma wa sekta binafsi katika kilimo kama Asasi za kiraia na  mashirika ya ndani na nje ya nchi yanayotoa huduma kwenye kilimo, wenye viwanda vya kuongeza thamani, watengenezaji, wauzaji na wasambazaji wa zana za kilimo n.k.

Amesema kuwa Usajili huo utafanyika kwa njia ya kidigitali  kwenye mtandao wa www.kilimo.go.tz na kupitia  simu za kiganjani.

Waziri Hasunga amesema kuwa Usajili huo utaanza rasmi tarehe 15 Februari, 2020 na kukamilika tarehe 14 Aprili, 2020.

Kupitia usajili huo, takwimu na taarifa muhimu zitapatikana kwa ajili ya kuendeleza kilimo zikiwemo watoa huduma za pembejeo, huduma za ugani, taasisi za fedha, wasindikaji na wenye viwanda, watengenezaji, wauzaji, wasambazaji wa zana za kilimo, na hivyo, kuweza kujua kiwango cha uwekezaji katika sekta ya kilimo.

Mhe Hasunga amesema kuwa Wizara ya kilimo inaendelea na usajili wa wakulima kote nchini ili kuweza kuwatambua na kurahisisha utoaji wa huduma za ugani, mitaji kwa ajili ya kilimo, upatikanaji wa pembejeo na kupata taarifa sahihi za uzalishaji.

Amesema kuwa Usajili wa wakulima Awamu ya Kwanza hadi kufikia Januari, 2020 umefikia jumla ya wakulima 1,279,884 na usajili unaendelea.

Kati yao, wakulima wa mashamba makubwa ni 147 wakewemo 101 wa zao la kahawa, chai 12, Mkonge 22 na miwa 12; na wakulima wadogo ni 1,279,737 wakiwemo 309,000 wa zao la Korosho (98.4%), 305,260  wa Kahawa (95.4), Pareto 10,687 (112%), Mkonge 6,885 (91%), miwa wakulima 6,745 (96.4), chai wakulima 31,092%, Tumbaku wakulima 53,757 (107.5%) na Pamba wakulima 556,306 (92.7).

Usajili wa wakulima Awamu ya Pili utaanza kwa kutumia mfumo wa kidigitari kwa kusajili taaarifa muhimu za wakulima ikiwemo ukubwa wa mashamba yao, aina ya teknolojia wanazotumia katika uzalishaji, wadau wanatoa huduma za kifedha, huduma za ugani, pembejeo, n.k

Waziri Hasunga amesema kuwa Maendeleo ya Kilimo hasa katika kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima yanategemea kwa kiasi kikubwa matumizi sahihi ya mbegu bora, mbolea na viuatilifu.

Licha ya umuhimu huo, bado kuna changamoto ya upatikanaji na matumizi sahihi ya pembejeo hizo ikilinganishwa na mahitaji.

Aidha, inakadiriwa kuwa wakulima nchini wanapoteza takribani asilimia 30 ya mazao kabla na baada ya mavuno kutokana na magonjwa na milipuko ya visumbufu mbalimbali vya mimea.

MWISHO



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com