Aliyekuwa Meneja wa Chama cha Ushirika cha 'Ngara Farmers Cooperative' mkoani Kagera, Hamphrey Kachecheba mwenye umri wa miaka 50 anadaiwa kujiua akiwa katika nyumba ya kulala wageni kwa kile kinachodaiwa ni msongo wa mawazo, kisa deni la shilingi milioni 889.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi amesema kuwa walipata taarifa kutoka kwa Meneja na mhudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni iliyopo eneo la Hamugembe, Manispaa ya Bukoba kuwa kuna mteja wao amejifungia chumbani na wakiita haitiki na walipofika walilazimika kuvunja mlango na kumkuta tayari amepoteza maisha.
Kamanda Malimi amesema walipofanya upekuzi katika chumba alimokuwa amelala walikuta barua ya kufukuzwa kazi na mwajiri wake ambaye ni 'Ngara Farmers Cooperative' kutokana na upotevu wa fedha shilingi milioni 889. Pia walikuta kifungashio ambacho ndani yake kilikuwa na dawa ambayo haijafahamika pamoja na chupa yenye kimiminika chenye rangi kama ya kijani na vitu vyeusi.
Mmoja wa wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni aliyejitambulisha kwa jina moja la Nyakato, amesema kuwa alikwenda na kugonga mlango asubuhi kwa lengo la kufanya usafi na kumdai hela ya chumba, na kuwa baba huyo aliitika na kumwambia ampelekee bia moja.
Naye mmiliki wa nyumba hiyo, Robert Katunzi amedai kuwa alipewa taarifa na mfanyakazi wake kuwa mteja wao ambaye amekuwa pale kwa muda wa siku nne, hafungui na hawana tena mawasiliano naye.
Chanzo - EATV
Chanzo - EATV