Wizara ya afya ya Misri imetangaza kisa cha kwanza kilichothibitishwa cha mgonjwa wa virusi vya Corona kinachokuwa cha kwanza pia barani Afrika.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema mgonjwa aliyebainika siyo raia wa Misri lakini pia haikufafanua uraia wa mtu huyo.
Maafisa wa Misri walifanikiwa kuthibitisha kisa hicho kupitia mpango ulioanzishwa na serikali wa kuwafuatilia abiria waliowasili kutoka nchini ambazo virusi vya Corona tayari vimesambaa.
Msemaji wa wizara ya afya ya Misri, Khaled Megahed, amesema serikali imechukua hatua za tahadhari na inafuatilia kwa karibu afya ya mgonjwa huyo ambayo imeripotiwa kuwa imara.
Mamlaka za Misri pia zimeliarifu shirika la afya duniani WHO kuhusiana na kisa hicho na tangu wakati huo mgonjwa huyo amewekwa karantini katika hospitali maalum ya umma.
Mahusiano ya karibu na China na mifumo dhaifu ya afya ni masuala yanayozua wasiwasi kuhusu uwezo wa nchi za Afrika wa kukabilina na mripuko wa virusi vya Corona vinavyyowauwa maelfu ya watu nchini China.
Hayo yanajiri wakati China imetangaza kuwa maambukizi ya virusi vya Corona yamefikia visa 66,492 huku idadi ya waliokufa imepanda hadi watu 1,523 na wagonjwa wengine 11,053 wako kwenye hali mahututi.
Social Plugin