Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DAKTARI ALIYETOA TAHADHARI YA VIRUSI VYA CORONA KWA MARA YA KWANZA NA KUPUUZWA AFARIKI DUNIA

Li Wenliang aliambukizwa virusi wakati akiwa katika hospitali ya Wuhan


Daktari raia wa China aliyejaribu kutoa tahadhari kuhusu mlipuko wa virusi vya corona amefariki, hospitali iliyokuwa ikimpatia matibabu imeeleza.

Li Wenliang alipata maambukizi wakati akifanya kazi katika hospitali mjini Wuhan.

Alituma ujumbe wa tahadhari kwa madaktari wenzake tarehe 30 mwezi Desemba lakini polisi walimuamuru kuacha ''kutoa taarifa na maoni ya uongo''.

Kulikuwa na ripoti za kukanganya kuhusu kifo chake, lakini inadaiwa na vyombo vya habari kuwa alifariki usiku wa kuamkia Ijumaa.

Virusi vimeua watu 636 na watu 31,161 wana maambukizi nchini China, tume ya taifa ya afya ilieleza kwenye takwimu zake za hivi karibuni.

Vifo hivyo vinahusisha 73 walioripotiwa siku ya Alhamisi.
Ilikuwaje kwa Li Wenliang?

Dokta Li, aliweka habari kwenye mtandao wa Weibo akiwa kitandani hospitalini mwezi mmoja baada ya kutuma ujumbe wa tahadhari.

Daktari huyo mwenye miaka 34 aligundua visa saba vya maambukizi ya virusi ambavyo alifikiri kuwa vilifananana Sars- mlipuko uliowahi kutokea mwaka 2003.

Tarehe 30 mwezi Desemba alituma ujumbe kwa madaktari wenzake akiwatahadharisha kuvaa vifaa vya kujikinga kuepuka maambukizi.

Siku nne baadae aliitwa na idara ya usalamaambapo aliamriwa kusaini barua. Katika barua hiyo alikuwa akishutumiwa ''kutoa taarifa za uongo'' ambazo zimeleta taharuki miongoni mwa jamii''.

Alikuwa mmoja kati ya watu nane ambao polisi walisema walikuwa wakichunguzwa kwa makosa ya ''kueneza uzushi'' mamlaka baadae zilimuomba radhi Dokta Li.

Katika taarifa aliyoiweka kwenye mtandao wa Weibo alieleza namna alivyoanza kukohoa mwezi Januari, siku iliyofuata alipata homa na siku mbili baadae alikuwa hospitalini. Aligundulika na virusi vya Corona tarehe 30 mwezi Januari.
Vifo vya watu wawili vitokanavyo na corona nje ya China vimeripotiwa

Raia wa nchini China wamepokeaje?

Ghadhabu na huzuni zilitanda kwenye mtandao wa kijamii wa Weibo pale taarifa za kifo cha Dokta Li zilipotangazwa siku ya Alhamisi.

Hashtag zikisema ''Serikali ya Wuhan inapaswa kumuomba radhi Dokta Li'' na ''tunataka uhuru wa kujieleza''.

Ujumbe wote huo ulianza kufuatiliwa na BBC ilipoanza kufuatilia mtandao wa Weibo siku ya Ijumaa asubuhi ikakuta ujumbe wa kampeni hizo na maoni yakiwa yameondolewa.

Sasa wengi wamekuwa wakiandika ujumbe wa kukosoa serikali bila kumtaja dokta Li moja kwa moja- lakini yote haya yanadhihirisha hasira ya raia wa China dhidi ya serikali.

''Usisahau jinsi unavyojisikia hivi sasa. Usisahau hasira hii. Hatupaswi kuacha hili litokee tena,'' mtu mmoja alieleza kwenye mtandao wa Weibo.

''Ukweli siku zote utaelezwa kuwa habari ya uzushi. Mpaka lini mtadanganya? Bado mnadanganya? kitu gani kingine mnachopaswa kuficha?'' mwingine alisema.
Kwanini kuna mkanganyiko kuhusu kifo chake ?

Gazeti la kila siku la Global times na vyombo vya habari vingine nchini China viliripoti kifo cha Dokta Li siku ya Alhamisi.

Global Times liliandika katika ukurasa wake wa twitter ukisema kuwa kifo cha Dokta Li kimeleta ''majonzi nchini China''

Waandishi wa habari na madaktari ambao hawakutaka kutajwa majina yao waliiambia BBC kuwa maafisa wa serikali waliingilia kati.

Vyombo vya habari rasmi viiambiwa vibadilishe ripoti zao ziseme kuwa daktari bado anapata matibabu.

Vyombo vya habari baadae viliripoti muda mwingine wa kifo cha Dokta Li.
Hali ya maambukizi hivi sasa

Ingawa virusi vimesambaa mpaka nje ya China, kukiwa na ripoti ya maambukizi kwenye mataifa 25, mpaka sasa kumeripotiwa vifo viwili nje ya China- mtu mmoja Hong Kong na mtu mmoja Ufilipino.

Shirika la afya duniani, WHO limetangaza mlipuko wa virusi vya corona kuwa janga la kiafya, likisema ikiwa fedha hazitaelekezwa kupambana na mlipuko, mataifa yatajutia hilo baadae.

Ingawa takwimu rasmi nchini zinasema kuna maambukizi 31,000, baadhi ya wanasayansi wamekisia kuwa idadi inaweza kuwa mara 10 zaidi, kwa kuwa wengi wao huonyesha dalili polepole, na hawapati matibabu, na hivyo kuwaambukiza wengine.
CHANZO- BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com