KatibuMkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Silas Shemdoe akiongea na Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
KatibuMkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Silas Shemdoe akisalimia na Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
Watendaji Wakuu wa Taasisi Mbalimbali wakimsikiliza Prof. Riziki Silas Shemdoe (Mbele kulia) Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Prof. Riziki Shemdoe ameweka bayana adhama yake ya kujikita katika utekelezaji wa sera ya Tanzania ya Viwanda.
Prof Shemdoe amebainisha hayo leo Januari 3, 2020 alipokutana na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Wakala zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwenye kikao kilichofanyika katika ofisi ndogo ya Wizara iliyopo waterfront Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kumuamini na kumpatia dhamana hiyo ambayo hakuitarajia.
“Namshukuru Mwenyezi MUNGU na Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa kuniamini na kuniteua kuwa Katibu mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo imebeba dhima ya kuwa na uchumi wa Viwanda”. Alisema Prof Shemdoe.
Aidha amewataka Watendaji Wakuu wa Taasisi na Wakala zilizo chini ya Wizara hiyo kujipanga kisawa sawa, kutambua wajibu mkubwa walionao kwa Tanzania na Zaidi ya yote kwenda na kasi ya Rais Magufuli.
“Ninachotaka kuwasisitiza ni kuwa Tufanye kazi ili kwenda na kasi ya Mhe. Rais wetu ambayo ni kuwa na Tanzania ya Viwanda. Tujue kuwa tumepewa jukumu kubwa sana hivyo yatupasa kushirikiana ili kuyafikia malengo ya Mhe. Rais ambayo anategemea katika Wizara yetu tuyafanye.
Nae Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Dkt. Manege Ludovick amemshukuru Katibu Mkuu Mteule Prof. Shemdoe kwa niaba ya maafisa watendaji wakuu wa waliofika hapo na kumuahidi kumpa ushirikiano “ wewe ni Kiongozi wetu tunakuahidi kukupa ushirikiano ili kufikia malengo ya Wizara na nchi kwa ujumla ya kuwa na Tanzania ya viwanda.
Prof. Shemdoe ameapishwa leo rasmi na Rais Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda ya Biashara ambapo kabla ya uteuzi huo alikua Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma.
Social Plugin