Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Anjela Kairuki, amesema ofisi yake imepata wawekezaji wakubwa wawili ambao wameonyesha nia ya kuwekeza katika kilimo ikiwamo kuchakata mafuta ya bangi kwa ajili ya matibabu.
Kairuki alikuwa akimpa taarifa mchangiaji aliyekuwa akichangia mjadala wa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mbunge wa Kahama Mjini (CCM), Jumanne Kishimba, aliyetaka serikali ipitishe jambo hilo mapema kabla bei ya bangi haijaporomoka.
Kishimba wakati anachangia mjadala huo alisema bei ya bangi duniani imepanda maradufu na nchi zote alizozizunguka wamesharuhusu kilimo cha zao hilo, hivyo anamwomba Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, atoe ufafanuzi kwamba watu wanaotaka kulima wamuone nani.
“Waliopiga marufuku bangi ni Wazungu miaka ya 40, lakini Wazungu walewale waligundua ndani ya bangi kuna dawa, na sisi wenyewe tunaenda kwenye viwanda vya dawa. Je, sisi tuki- import dawa zenye material ya bangi (tukiagiza dawa zenye malighafi itokanayo na bangi) tutakuwa tumeagiza kutoka wapi na tuta declare (kutangaza maslahi) namna gani. Kwa kuwa bei ya masoko duniani ni bei ya ushindani… ni vizuri serikali ifanye uamuzi huo mapema zaidi.
Kishimba aliongeza: “Tanzania kwa Afrika ni nchi ya tatu kwa kulima bangi kwa magendo na kama wataruhusu na sheria kama ilivyo inaweza sana ikatusaidia kutupeleka mahali. Lakini kwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi (George Simbachawene) yuko hapa anaweza akatoa msamaha hata kwa bangi iliyokamatwa kwa muda wa miezi sita, kama msamaha anavyoutoa wa silaha.”
Kwa mujibu wa Kishimba, msamaha huo kama utatolewa na wananchi wakawasilisha bangi hizo Polisi, watu wakauziana bangi hiyo Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) watapata mapato na wanunuzi wakaja kununua hapa, linaweza kusaidia wenzetu wakapata pesa na kwa hali hiyo, lazima tuende haraka sana.
“Uganda wamepewa na Jumuiya ya Nchi za Ulaya (EU), zaidi ya Dola milioni 500 kwa ajili ya kilimo cha bangi, na kwamba kwa kuwa tulianza kulima bangi muda mrefu, lakini basi namuomba waziri wakati wowote kama watapitisha iwe mapema kabla bei haijaporomoka,” alisema.
Wakati Kishimba anachangia mjadala huo, Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma alisimama na kumpa taarifa akisema:
“Kikawaida Bunge linapotunga sheria kinachofuata ni kanuni tu, sasa nilikuwa nafikiria Mheshimiwa Waziri angetuambia kanuni ziko tayari ili tuanze kulima kwa sababu bangi itaporomoka bei.”
Baada ya michango hiyo ya wabunge, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema: “Niwa assue this is not a joke (niwahakikishie kwamba hili sio jambo la utani), anachochangia (Kishimba)… nilikuwa Canada majuzi hapa kwenye mkutano wa ma Spika wa Common Wealth (Jumuiya ya Madola) duniani. Ni big business in Canada (Ni biashara kubwa). Kwa hiyo anazungumza kitu cha msingi sana wala sio utani.
“Tena linaweza kuwa ni zao kubwa la biashara linaoweza kundoka kuliko mazao mengi tu kabisa, likafanya mapinduzi makubwa sana ya kipato. Kwa hiyo anachokizungumza Mheshimiwa Kishimba hazungumzi bangi itumike vile ambavyo tunavyofahamu inatumika hapa nchini.
“Tunazungumzia habari ya kilimo, moderated, monitored na taratibu zote halafu wanapelekewa wote wanaohitaji kwa ajili ya kutengeneza dawa za wanyama na binadamu.”
Social Plugin