Na Mwandishi Wetu,
Maboresho katika sekta ya afya yanayoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, yamewafanya raia kutoka nchi jirani ya Kenya kumiminika nchini kwa ajili ya kupata matibabu.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la nchini Kenya la Februari10, 2020, raia wa Kenya hasa wanaoishi Mji wa Taveta ulipo mpakani mwa Tanzania nan chi hiyo wamekuwa wakivuka mpaka kuja nchi kutokana na huduma bora na nafuu zinazotolewa na hospitali ya KCMC na Kituo cha Afya cha Himo mkoani Kilimanjaro.
Gazeti hilo linamtaja Bw. Patrick Mnyange ni miongoni mwa wagonjwa waliopatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Himo baada ya kushambuliwa kwa mapanga nchini Kenya Disemba 2019 na kushindwa kupata matibabu stahiki nchini kwake hali iliyoilazimu familia yake kumsafirisha hadi Tanzania kupata matibabu ambapo alilazwa kwa mwezi mzima hadi aliporuhusiwa mwezi Januari mwaka huu.
"Tungeweza kumpoteza kwani alikuwa anavuja damu sana na alihitaji matibabu ya haraka na ndipo tulipoamua kumleta Tanzania. Sasa hivi anaendelea vizuri," anasema mke wa Mnyange, Bi. Floice Rusiana.
Bi. Floice anasema kuwa kwa kipindi cha mwezi mmoja alichokuwa amelazwa mume wake, kuna wagonjwa wengine nane kutoka Kenya walikuwa pia wamelazwa hapo. "Wengine walitokea Werugha, Kasigau, Voi na Mji wa Taveta town, wote tulikuwa nao katika Wodi moja," anaeleza.
Gazeti la Daily Nation linamtaja Bw. Juma Miraj kutoka kijiji cha Bura Ndogo nchini Kenya, akieleza jinsi mpwa wake alivyopatiwa matibabu ya upasuaji wa kuondoa uvimbe tumboni katika hospitali ya Rufaa KCMC iliyopo Kilimanjaro kwa gharama nafuu.
Kwa mujibu wa mwandishi wa taarifa hii kutoka gazeti la Daily Nation, Lucy Mkanyika, raia hao wa Kenya wanakuja Tanzania kupatiwa matibabu ya kibingwa kutokana na uboreshwaji wa huduma na gharama nafuu kulinganisha na nchini Kenya
Social Plugin