Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amewaasa watumishi wa Ofisi yake kuendelea kuzingatia sheria na kanuni za utumishi wa umma katika utendaji kazi wao ili kuendelea kuitumikia nchi kwa weledi na ufanisi na kufikia malengo kwa wakati unaostahili.
Ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha kwanza cha mwaka cha Baraza la Wafanyakazi la Ofisi hiyo kilichofanyika Februari 3, 2020 Jijini Dodoma.
Waziri Mhagama aliwataka watendaji wote kuona umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa weledi huku wakizingatia sheria za utumishi wa umma ikiwemo nidhamu kazini, kauli nzuri kwa wateja, kuzingatia mavazi ya staha na kuwahi kazini.
Waziri aliongezea kuwa, ni lazima mtumishi wa umma afanane na kanuni na sheria za kiutimishi kwa kuwa na maadili mazuri awapo kazini na nje ya kazi ili kujipatia sifa njema kuanzia muonekano hadi tabia kwa ujumla.
“Hatutegemei mtumishi wa umma tena wa ofisi hii anakuwa ndiye mlevi wa kupindukia yaani ndiye namba moja Dodoma hii , wala kuvaa mavazi yasiyoendana na hadhi ya utumishi wa umma, hiyo kwetu hatutoivumilia lazima tuikatae na kuhakikisha tunakuwa mfano wa kuingwa,”Alisistiza
Waziri aliwakumbusha watendaji wa ofisi hiyo kuzingatia nafasi zao za kiutendaji wawapo kazini kwa kuzingatia jukumu la ofisi yake ni Kuratibu Shughuli zote za Serikali hivyo lazima iwe ofisi ya mfano.
“Ofisi yetu inaratibu shughuli zote za Serikali , muone ni kwa namna gani sisi ni viungo kwa Serikali hii hivyo mtumie fursa ya baraza hili kukumbushana wajibu wetu kwa kuhakikisha mnatekeleza majukumu kwa nidhamu ya hali ya juu sana,”alisema Waziri Mhagama
Aliutaka uongozi pia kuendelea kuwa na umoja na kufanya kazi kwa kuzingatia dhana ya ushirikishwaji ili kujenga tija kwa kupitia vikao ambavyo vitaibua changamoto zinazowakabili pamoja na kuishauri vyema Serikali kuhusu usimamizi wa kazi na rasilimali watu tunayoisimamia kila siku.
“Ni muhimu kuwa na vikao ili kuendelea kusimamia ustawi sehemu zetu za kazi, na uwepo wa mabaraza haya utaleta tija kwa kuzingatia mchango wake kwa Serikali nzima na hakikisheni mnayatumia kwa kuzingatia dhana ya ushirikishaji,”alieleza Waziri
Aidha aliongezea kuwa ni muhimu viongozi wote kuanzia ngazi ya Vitengo, Idara na Taasisi zote kuendelea kusimamia utekeleaji wa majukumu kwa kufuata sheria, miongozo na kanununi za utumishi wa umma huku wakiwa na upendo kati yao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Baraza hilo Bw. Tixon Nzunda aliahidi na kumhakikishia Waziri kuwa, watatekeleza maagizo na maelekezo aliyoyatoa ikiwa ni pamoja na kuzingatia maadili mazuri na kuahidi kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa ofisi hiyo juu ya utoaji wa huduma bora inayozingatia viwango vya hali ya juu.
“Tunakushukuru Waziri na nikuhakikishie kuwa unatimu imara, tulivu na chapakazi na tutatekeleza maagizo yote kwa kasi ya mabadiliko ya hali ya juu,”alisema Bw.Tixon
Naye mmoja wa wajumbe wa baraza hilo Bi. Numpe Mwambeja alieleza furaha yake kwa kumshukuru Waziri kwa maelekezo yake yenye nia njema ya kuendelea kuona ofisi yake inakuwa ya mfano katika utendaji kazi wa kila siku na kuahidi kuzingatia maagizo aliyoyatoa.
“Kwa niaba ya wajumbe wenzangu wa kikao cha baraza nimefarijika sana na maagizo yaliyotolewa na waziri ikiwemo kuzingatia suala la uadilifu, kuwahi kazini, kuvaa mavazi ya staha, kuacha uvivu na kuwa na kauli nzuri katika hudumia wateja wa ndani na nje ya ofisi ili kufanya kazi zetu kwa ufanisi unaotakiwa,”alisema, Numpe.
Social Plugin