WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kila raia wa Tanzania aliyeomba kitambulisho cha Taifa atakipata, hivyo amewataka waombaji ambao bado hawajapata waendelee kuwa na subira.
Amesema waombaji hao watapatiwa vitambulisho hivyo baada ya wahusika kupitia maombi yao na kujiridhisha kwamba wote ni raia wa Tanzania na Serikali inafanya hivyo ili kulinda usalama wa nchi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 21, 2020) wakati akizungumza katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kigoma. Waziri Mkuu ni mlezi wa CCM wa mkoa wa Kigoma.
“Watu wote wanaotaka kuingia nchini ni lazima wafuate taratibu zilizowekwa pia Uhamiaji na vyombo vingine vya dola vijiridhishe kwamba hata hao wanaopitia njia sahihi kama kweli ni watu wema.”
Waziri Mkuu amesema katika mikoa ya mipakani ina tatizo la watu kuingia bila ya kufuata taratibu, hivyo kabla ya kutoa kitambulisho ni lazima Serikali ijiridhishe kama kweli aliyeomba ni raia. “Pale wahusika watakapohitaji kujiridhisha waombaji watoe ushirikiano.”
Waziri Mkuu amesema lazima zoezi hilo lifanyike vizuri na wataharakisha ili wananchi waweze kupata vitambulisho. Tayari Serikali imeshaongeza vifaa na watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili waweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Akizungumzia kuhusu taarifa baadhi ya wananchi wakuombwa rushwa ili waweze kupata vitambulisho, Waziri Mkuu amewataka watu wote walioombwa rushwa wakaripoti katika vyombo vya sheria. Amesema marufuku mtu kuomba wala kupokea rushwa.
Waziri Mkuu amesema kuwa suala la kuimarisha ulinzi na usalama katika mikoa ya mipakani ukiwemo na mkoa wa Kigoma ni jambo muhimu kwa sababu bila ya kuimarisha ulinzi mikoa hiyo haitakweza kupata maendeleo. Amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka viongozi na wanachama wa CCM washirikiane na wabunge na madiwani waliopo sasa na wasiwavuruge wawaache watekeleze majukumu yao hadi pale muda wao utakapomalizika.
Pia, Waziri Mkuu amewataka viongozi na wanachama wa CCM wajiepushe na suala la ukabila na udini katika kuteua mtu wa kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho na badala yake wateue mtu ambaye anauzika ndani na nje ya chama.
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
Social Plugin