Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU: SERIKALI HAINA LENGO LA KUMKOMOA MTU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeagiza umakini ufanyike katika utoaji wa vitambulisho vya Taifa hususani katika mikoa ya mipakani si kwa lengo la kutaka kumkomoa mtu bali ni kwa ajili ya kuimarisha usalama wa nchi.


Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Februari 20, 2020) baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wabunge wa mkoa wa Kagera kuhusu usumbufu wanaoupata baadhi ya wananchi wanapofuatilia vitambulisho vya Taifa kwani wengine wanadaiwa kuwa si raia.

Malalamiko hayo yametolewa wakati Waziri Mkuu akizungumza katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kagera. Waziri Mkuu ni mlezi wa CCM wa mkoa wa Kagera.

“Watu fuate taratibu katika suala ugawaji wa vitambulisho, Idara ya Uhamiaji wafuatilie kwa umakini kwa sababu lazima usalama wa nchi usimamiwe ipasavyo hususani katika mikoa ya mipakani. Watanzania mnatakiwa muwe makini msiruhusu watu kuingia kwa njia za panya kwani watu hao hawana nia njema.”

Waziri Mkuu amesema lazima zoezi hilo lifanyike vizuri na wataharakisha ili wananchi waweze kupata vitambulisho. Tayari Serikali imeshaongeza vifaa na watumishi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili waweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka viongozi na wanachama wa CCM waimarishe mshikamano miongoni mwao na pale kwenye dosari zirekebishwe kwa sababu hakuna jambo lisiloweza kutatuliwa.

“Tunahitaji kuwa na umoja na mshikamano ndani ya chama ili sote kwa pamoja tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea….Hata katiba yetu ya chama inatuhimiza tushikamane kwani wote tunajenga nyumba moja hivyo hatuna sababu ya kugombea fito.”

Waziri Mkuu amesema lazima wahakikishe kuwa chama cha CCM kinabaki salama na kinaendelea kushika dola. “Ni wajibu wa kila kiongozi na mwanachama kuwezesha malengo hayo kutimia na ni lazima kila tawi litafakari namna ya kukiwezesha chama kujitegemea kiuchumi.”

Pia, Waziri Mkuu amewataka viongozi na wanachama wa CCM wajiepushe na suala la ukabila na udini katika kuteua mtu wa kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho na badala yake wateue mtu ambaye anauzika ndani na nje ya chama.

(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com