WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaasa wanasiasa nchini kutotumia mlipuko wa virusi vya corona uliotokea China na kuua watu zaidi ya 1,400 kujipatia umaarufu wa kisiasa.
Hivyo, Waziri Mkuu amewataka Watanzania waendelee kuitegemea Serikali katika kupata taarifa za mara kwa mara kuhusu masuala mbalimbali zikiwemo na za mlipuko wa virusi hivyo. “Tusiupoteshe umma.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 14, 2020) mara baada ya kushiriki swala ya Ijumaa katika msikiti wa Gaddafi, jijini Dodoma. Amesisitiza umuhimu wa wananchi kuliombea Taifa ili Mwenyezi Mungu aliepushe na maafa mbalimbali.
Waziri Mkuu amesema kazi inayofanywa na Serikali kwa sasa nchini ni kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama, ambapo ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi waendelee kumuomba Mwenyezi Mungu aliepushe Taifa na maafa mbalimbali ikiwemo mlipuko wa corona, baa la nzige na mafuriko
Amesema katika mji wa Wuhan ambako virusi hivyo vilianzia, wapo vijana 497 wa Kitanzania huko na wote wapo salama na Serikali inaendelea kuwasiliana nao kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na ofisi za ubalozi.
“Taifa hili ni muhimu sana kwetu na ni msingi wa maisha yetu, hivyo watu wasiwe wanapotosha umma na kuwatia hofu Watanzania, vijana wetu wapo salama. Pia tumejipanga kukabiliana na majanga hayo ikiwa ni pamoja na nzige. Tumuombe sana Mwenyezi Mungu atuepushe”
Kadhalika,Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi wawasikilize viongozi wa dini na waendelee kumuomba Mwenyezi Mungu awape uvumilivu na waliombee Taifa lidumishe amani.
“Viongozi wa dini muendelee kuhamasisha uwepo wa amani nchini. Taifa linaendelea kuwa na amani kutokana na mawaidha yanayotolewa na viongozi mbalimbali wa dini.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Wanzania waendelee kushikamana na wafuate maelekezo yanayotolewa na viongozi wa dini ili waweze kujenga msingi imara kwa vijana.
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
Social Plugin