WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi Desema 2019, ujenzi wa reli ya kati ya kisasa (Standard Gauge) kwa sehemu ya Dar es Salaam – Morogoro (kilometa 300) umefikia asilimia 70.
Amesema hatua hiyo ni miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Desemba, 2019.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Februari 7, 2020) wakati akiahirisha mkutano wa 18 wa Bunge la 11 bungeni jijini Dodoma. Amesema mafanikio hayo yametokana na kuimarika kwa mapato.
Amesema kazi za ujenzi kwa sehemu ya Morogoro – Makutupora (kilometa 422) zinaendelea vizuri na Serikali imerejesha huduma ya reli ya abiria na mizigo ya Kaskazini (Dar es Salaam – Moshi).
Waziri Mkuu ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuendelea na ujenzi wa Mradi wa kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere ambapo kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa daraja la muda namba 2; utafiti wa miamba na udongo; uchimbaji wa mtaro wa chini kwa chini wenye urefu wa mita 147.6.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imefanikiwa kuendeleza Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) ambapo hadi Desemba 2019 jumla ya vijiji 8,236 kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara vimeunganishwa na umeme, sawa na asilimia 67.1.
“Aidha, kufuatia malalamiko ya ucheleweshaji wa baadhi ya miradi ya REA, namuagiza Waziri wa Nishati kuhakikisha wakandarasi wote kwenye mpango wa REA wanakamilisha majukumu yao kwa wakati,” amesema.
Kuhusu usafiri wa anga, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuboresha Shirika la Ndege Tanzania kwa kununua ndege mpya 11. “Hadi Desemba 2019, ndege 8 zimepokelewa na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege nyingine mpya tatu yameshafanyika.”
“Kuzinduliwa kwa Jengo la Tatu la abiria katika kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere na kuanza kutumika kuhudumia abiria; kuendelea na uboreshaji wa kiwanja cha ndege Mwanza na viwanja vya mikoa mbalimbali.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo barabara kuu, barabara za mikoa na za wilaya. Mtandao wa barabara kuu umefikia kilometa 8,502 na mtandao wa barabara za mikoa kilometa 1,756.
Pia, Serikali imeendelea na ujenzi wa Ubungo inter-changeambapo hadi Desemba 2019 ulifikia asilimia 62 na ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha umefikia asilimia 63.
Kuhusu miundombinu ya madaraja Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kukamilisha ujenzi wa madaraja ya Sibiti (Singida), Momba (mpakani mwa Songwe na Rukwa), Mlalakuwa (Dar es Salaam), Lukuledi (Lindi) na kuendelea na ujenzi wa daraja la Selander na daraja la Kigongo – Busisi lenye urefu wa mita 3,200 na upana wa mita 28.45.
“Mbali na hayo tunaendelea na ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 37; ujenzi wa chelezo umefikia asilimia 46; ukarabati wa meli ya MV Victoria umefikia asilimia 65 na MV Butiama asilimia 60.”
Amesema hatua nyingine inayochukuliwa na Serikali ni kukamilika kwa ujenzi wa kivuko kipya cha Kigongo – Busisi; kuendelea na ujenzi wa kivuko kipya cha Nyamisati – Mafia; kuendelea kukarabati vivuko vya MV Sengerema (asilimia 40); MV Kigamboni (asilimia 60), na MV Utete (asilimia 95).
Akizungumzia kuhusu bandari ya Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema upanuzi wa bandari hiyo unaendelea ambapo ujenzi wa gati namba moja, mbili na tatu pamoja na gati la kupakia na kupakua magari (Ro-Ro) umekamilika.
Waziri Mkuu amesema kukamilika huko kwa gati la kupakia na kupakua magari kutawezesha meli ya kwanza yenye uwezo wa kubeba magari 6,000 kuhudumiwa katika gati hilo. Uboreshaji wa bandari za Tanga, Mtwara na bandari za maziwa makuu pia unaendelea.
(mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
Social Plugin