Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI UMMY AWATAKA WAZAZI KUWEKEZA KATIKA AFYA ZA WATOTO

Na Mwandishi Wetu Dar Es Salaam

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewataka wazazi kuwekeza kwa watoto katika kupata huduma bora za afya ili kuwawezesha kupata elimu bora itakayowasaidia watoto kutimiza malengo yao.

Waziri Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua akaunti za watoto na vijana zinazojulikana kama Malaika, Janja, Kizazi Kipya na Hazina za Benki ya UBA ambazo zimetengenezwa kulingana na umri wa watumiaji.

“Nitumie fursa hii kuwahimiza walezi na wazazi wa watoto kuwa na utaratibu wa kuweka akiba kwa elimu ya watoto wetu. Hii itasaidia kufikiwa kikamilifu kwa haki ya kuendelezwa mtoto” alisema Waziri Ummy

Waziri Ummy ameiomba Benki ya UBA kuunganisha huduma za akaunti za watoto na huduma ya Bima ya Afya ili kuwezesha watanzania waliowengi kuweza kupata huduma za afya hasa kwa watoto ambao wamekuwa na changamoto nyingi za kiafya hasa katika ukuaji wao.

 “Nawapongeza kwa ubunifu wa kuwa na akaunti hizo za watoto kulingana na rika, ila kama Waziri nawaomba muunganishe akaunti hizi na Bima ya Afya kwa watoto itakuwa masaada mkubwa kwa wazazi na walezi” alisema Waziri Ummy

Waziri Ummy aliutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuona namna ya kuunganisha huduma za akaunti hizo na Bima ya Afya kwasababu kwa watoto chini ya umri wa miaka kumi na nane wanaweza kujiunga kwenye huduma ya Watoto afya kadi ambapo inaweza kuwafikia watoto wengi.

Aidha Waziri Ummy aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Benki ya UBA Tanzania kwa kubuni huduma hizo mpya zinazoenda na umri wa watoto kwasababu itachangia maendeleo ya watoto na vijana.

“Nitumie fursa hii kuwapongeza Bodi na Menejimenti ya Benki ya UBA kwa kubuni bidhaa ambayo itachangia katika maendeleo ya watoto na vijana, muendelee na kasi hiyo ya utoaji huduma ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, mnatekeleza Sera ya Mtoto ya mwaka 2009 kwa kuwa inahimiza wazazi na walezi kutimiza haki ya msingi ya kuendelezwa kwa mtoto.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya UBA Tanzania, Usman Isiaka, akiongea katika uzinduzi huo alisema huduma hizo nimuendelezo wa falsafa ya Benki ya UBA ya kutoa huduma kulingana na uhitaji wa wateja, mahali wanapotaka na kwa njia wanayotaka kuipata huduma hiyo.

“Benki ya UBA Tanzania tuna mtazamo wa kutoa bidhaa na huduma mbalimbali kulingana na teknolojia na zilizo bora kwa wateja kwa lengo la kuboresha soko letu na ushindani katika Sekta ya kibenki nchini Tanzania.” Alisema Bw. Isiaka

Katika uzinduzi huo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alizindua huduma za akaunti ya Malaika ambayo inalenga watoto kuanzia umri wa siku moja mpaka miaka 12, akaunti Janja ni kwa watoto kuanzia miaka 13 mpaka 17 ambao wanakuwa kwenye shule za msingi na Sekondari, akaunti ya kizazi kipya inayolenga wanachuo na vijana wenye miaka 18 mpaka 25 na akaunti ya Hazina kwa watu wote wenye nia ya kujiwekea akiba kwa lengo la kutimiza lengo husika.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com