WANAWAKE KUONEANA WIVU, UWEZO MDOGO WA KUFANYA KAMPENI WAKWAMISHA WANAWAKE



Afisa Maendeleo halmashauri ya wilaya ya Kishapu Rehema Edson akizungumza kwenye warsha ya Jinsia,Uongozi na Demokrasia kwa lengo la kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika uongozi iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) iliyofanyika katika Ukumbi wa Bm Maganzo wilayani Kishapu leo Jumanne Februari 18,2020 na kukutanisha maafisa watendaji,viongozi wa serikali za mitaa wilayani Kishapu.Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Afisa Maendeleo halmashauri ya wilaya ya Kishapu Rehema Edson akizungumza kwenye warsha ya Jinsia,Uongozi na Demokrasia iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
Afisa Mtendaji wa kata ya Maweja, Samsom Masele akichangia hoja kwenye warsha hiyo ambapo alisema baadhi ya wanawake wana uwezo mdogo wa kufanya kampeni za uchaguzi lakini pia wanawake wamekuwa wakioneana wivu wao kwa wao wenzao wanapoomba nafasi za uongozi.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nshishinulu kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge,Esther Lugondeka akizungumza katika warsha hiyo ambapo alisema wanawake ni jeshi kubwa hivyo wanatakiwa kupendana,kushirikiana na kuwaunga mkono wanawake wenzao wanapojitokeza kugombea nafasi za uongozi ili wapate ushindi wa kishindo. 
Diwani wa Viti Maalumu kaya ya Ukenyenge, Josephine Malima akiwashauri wanawake kujihusisha na shughuli za ujasiriamali na kujiunga kwenye vikundi mbalimbali ili kujiimarisha kiuchumi wawe na fedha zitakazowasaidia kununua vitu vidogo vidogo huku akibainisha kuwa sasa jamii imeanza kubadilika na wanawake wameanza kushirikiana badala ya kubezana wao kwa wao.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mayanji kata ya Ukenyenge, Sheikh Othman Ndamo ambaye ni Sheikh wa kata ya Kishapu akiwasilisha kazi ya kundi lake.
Afisa Mtendaji kijiji cha Mwaweja  Charles Makwaya akiwasilisha kazi yake.
Washiriki wa warsha hiyo wakiwa ukumbini.
Washiriki wa warsha hiyo wakifanya kazi ya kikundi.
Washiriki wa warsha hiyo wakifanya kazi ya kikundi.
Washiriki wa warsha wakiwa ukumbini.

**
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Imeelezwa kuwa kitendo cha wanawake kuoneana wivu wao kwao pamoja na uwezo mdogo wa wanawake kufanya kampeni katika uchaguzi pamoja na unachangia wanawake kushindwa kupata nafasi za uongozi katika jamii. 

Hayo yamesemwa na wadau wa haki za wanawake leo Jumanne Februari 18,2020 kwenye warsha ya Jinsia,Uongozi na Demokrasia kwa lengo la kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika uongozi iliyoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) iliyokutanisha pamoja maafisa watendaji,viongozi wa serikali za mitaa na Afisa Maendeleo halmashauri ya wilaya ya Kishapu iliyofanyika katika Ukumbi wa Bm Maganzo wilayani Kishapu.

Afisa Mtendaji wa kata ya Maweja, Samsom Masele alisema baadhi ya wanawake wana uwezo mdogo wa kufanya kampeni za uchaguzi lakini pia wanawake wamekuwa wakioneana wivu wao kwa wao, mmoja akijitokeza kugombea nafasi ya uongozi wanawake wenzake wanaanza kumdhoofisha na kumkatisha tamaa na kusababisha nafasi zao katika uongozi ziwe chache. 

“Wivu baina ya wanawake kwa wanawake ni mkubwa sana,wanaowakatisha tamaa ni wanawake wenzao,wabezana wao kwa wao wanasema ndiyo tuongozwe na huyu? Wanachekaa na kugongeana,hii inarudisha sana nyuma”, alisema Masele.

Aidha alisema ili wanawake waweze kushika nafasi za uongozi,wanawake wanatakiwa wapewe elimu ya upigaji kampeni na wajengewe uwezo wa kujiamini kwa kuwapa elimu na uzoefu mbalimbali pamoja na kuwashirikisha kwenye ngazi za maamuzi 

Aliitaka jamii kuachana na mtazamo hasi juu ya kauli zinazomgandamiza mwanamke ikiwemo ile ya‘Mwanamke akiwa kiongozi atakuwa malaya’ akibainisha kuwa mtu yeyote anaposhika madaraka kiongozi lazima kuna mabadiliko yanajitokeza ikiwemo mavazi. 

“Ukiwa kiongozi lazima utabadilisha hata aina ya mavazi kutokana na hali hiyo wengi wanakuona umebadilika. Kama kioo wa jamii utahitajika kuwa na mabadiliko. Ukiwa kiongozi utakutana na watu mbalimbali kutokana na kwa hali hiyo wanawake wakimuona mwanamke anakutana na wanaume wanakuwa na fikra potofu kuwawanaume zao wanachukuliwa na huyo mwanamke kiongozi”,alisema Masele. 

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nshishinulu kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge,Esther Lugondeka alisema wanawake ni jeshi kubwa hivyo wanatakiwa kupendana,kushirikiana na kuwaunga mkono wanawake wenzao wanapojitokeza kugombea nafasi za uongozi ili wapate ushindi wa kishindo. 

“Baadhi ya wanawake wamekuwa wakiwabeza wanawake wenzao wanaojitokeza kugombea nafasi za uongozi kwa sababu ya kutojua wajibu wa wanawake endapo watakuwa viongozi.Kubezwa kunasababisha baadhi ya wanawake kukata tama na kuachana na nia ya kuwa viongozi”,alisema Lugondeka. 

Mwenyekiti wa kijiji cha Mayanji kata ya Ukenyenge, Sheikh Othman Ndamo ambaye ni Sheikh wa kata ya Kishapu alisema miongoni mwa sababu zinamkwamisha mwanamke kushika nafasi za uongozi ni kutokuwa na ujuzi wa kufanya kampeni na kushawishi wapate wapiga kura. 

“Wanawake wengi hawana ujuzi wa kupiga kampeni, Wanatakiwa wapewe elimu ya upigaji kampeni ili waweze kufikia malengo yao. Lakini pia Jamii ielimishwe kuondokana na mfumo dume ili kufikia hamsini kwa hamsini na kuongeza nafasi za uongozi”,alisema Sheikh Ndamo. 

Naye Diwani wa Viti Maalumu kaya ya Ukenyenge, Josephine Malima aliwashauri wanawake kujihusisha na shughuli za ujasiriamali na kujiunga kwenye vikundi mbalimbali ili kujiimarisha kiuchumi wawe na fedha zitakazowasaidia kununua vitu vidogo vidogo huku akibainisha kuwa sasa jamii imeanza kubadilika na wanawake wameanza kuwaunga mkono wanawake wenzao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post