Katibu Mkuu wa Madini, Profesa Simon Msanjila ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imeandaa mkutano wa kimataifa wa Madini na Uwekezaji unaotarajia kufanyika tarehe 22 na 23 mwezi Februari 2020 katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwl. J. K Nyerere jijini Dar es Salaam.
Amebainisha kuwa serikali imeamua mikutano hiyo kufanyika kila mwaka tarehe 22 na 23 ya mwezi Februari huku ikiwakutanisha wadau mbalimbali wa madini kutoka nchi mbalimbali duniani.
Profesa Msanjila ameyasema hayo leo tarehe 19 Februari alipokuwa kwenye mahojiano ya moja kwa moja yaliyofanyika kwenye studio za Televisheni ya Taifa (TBC 1) zilizopo jijini Dodoma katika kipindi cha ‘Jambo Tanzania’ Kinachorushwa kila siku kuanzia saa 12:00 hadi saa 2:00 Asubuhi.
Profesa Msanjila amesema Mkutano huu ni wa pili kufanyika baada ya ule uliofanyika Tarehe 22 na 23 Februari mwaka 2019 uliowakutanisha wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa wa madini nchini pamoja na wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa madini waliopo nchini.
Akizungumzia ukubwa wa mkutano huo wa kimataifa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, Profesa Msanjila alisema mkutano huo utahusisha nchi kumi na tano (15) na utakuwa na washiriki wasiopungua elfu mbili (2000).
Profesa Msanjila amesema, Wizara yake ikishirikiana na Taasisi zilizopo chini yake wanatarajia kupokea Mawaziri 12 kutoka nchi 12 za Maziwa Makuu ambao tayari wamekwisha thibitisha ushiriki wao katika mkutano huo mkubwa wa kimataifa kwa sekta ya madini.
Pamoja na mawasilisho ya mada mbalimbali na majadiliano ya pamoja, Profesa Msanjila amebainisha kuwa mkutano huo utakwenda sanjari na maonesho ya teknolojia ya uwekezaji na biashara ya madini ambapo wachimbaji wakubwa wataonesha namna bora ya uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini inavyofanyika kwa lengo la kuachilia uelewa na maarifa kwa wachimbaji wadogo wa madini.
Aidha, amebainisha kuwa katika Mkutano huo, kutakuwa na mikutano midogo midogo itakayokuwa ikiwakutanisha watu tofauti tofauti wakiwapo wenye mitaji kwa wasio nayo, wanaohitaji washirika katika kuwekeza eneo la uchimbaji wa madini, wanunuzi na wauzaji pamoja na makundi mengine mengi kwa kadri yatakavyojitokeza. Mikutano hiyo yote itaratibiwa na Wizara na Taasisi zake.
Akizungumzia malengo hasa ya Mkutano wa kimataifa kwa mwaka huu, Prof. Msanjila alisema ni kuwakutanisha wadau wa madini katika Nyanja tofauti tofauti ikiwemo wanaochimba madini, wale wanaotengeneza na kuuza tekinolojia, wadau wenye mitaji na wasionayo lakini pia kwa upande wa serikali kujifunza pale palipopungua ili kuweza kuboresha na kuifanya sekta ya madini kuwa ni sekta yenye tija kwa taifa.
Akielezea matokeo ya Mkutano wa kisekta wa mwaka 2019 Profesa Msanjila alisema ulipelekea mageuzi na maboresho makubwa katika sekta ya madini na kuifanya sekta kuongeza mchango wake kwenye pato la taifa.
Profesa Msanjila amebainisha mageuzi hayo kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini na kanuni zake, kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa wachimbaji wadogo wa madini, Kuondolewa kwa kodi ya zuio, Uboreshwaji wa miundombinu sehemu zinakofanyika shughuli za uchimbaji hususani Mirereni pamoja na uboreshaji wa kanuni mbalimbali zinazosimamia sekta ya madini.
“Mageuzi hayo yameufanya mchango wa wachimbaji wadogo wa madini kwenye pato la taifa kuongezeka kwa kasi na hiki ndicho tunachokitaka wizara ya Madini”. Alisisitiza.