Kikundi cha Wanawake na Mabadiliko mkoa wa Shinyanga (Women For Change - WFC) kinachojihusisha na Ununuzi wa Hisa ili kuinuana kiuchumi na chenye mfuko wa kusaidia jamii na watoto walioko kwenye mazingira magumu kimeandaa 'Tamasha la Shy Women's Day Out' kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani mwaka 2020.
Mwenyekiti wa Tamasha la Shy Women's Day Out, Faustina Kivambe amesema Tamasha hilo litafanyika siku ya Jumamosi Machi 7,2020 kuanzia saa 8 mchana katika ukumbi wa CCM mkoa wa Shinyanga /NSSF ya zamani ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko.
"Kabla ya Tamasha, Machi 5,2020 tutakabidhi bweni la watoto wa kiume katika kituo cha kulelea watoto wenye Ualbino cha Buhangija katika Manispaa ya Shinyanga tulilolifanyia ukarabati na mgeni rasmi atakuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga pamoja na wadau mbalimbali waliodhamini tamasha hili",amesema Kivambe.
"Siku ya Jumamosi Machi 7,2020 kuanzia saa 8 mchana tutakutana katika Ukumbi wa CCM mkoa wa Shinyanga/NSSF ya zamani kwa ajili ya Tamasha ambapo Kiingilio katika Tamasha hilo ni Shilingi 30,000/=. Tiketi zinapatikana katika duka la Fk House of Kids na CPK Gas Point nyuma ya Benki ya CRDB au piga simu namba 0758 016 162 au 0759 725 898",ameongeza Kivambe.
Amesema Tamasha hilo pamoja na uwepo wa burudani,chakula na vinywaji pia litaongozwa na mada mbalimbali ikiwemo Ujasiriamali, Mahusiano,Ndoa na Malezi, Ushauri wa kisheria na afya.
Amewataja watoa mada kutoka ndani na nje ya Shinyanga watakuwepo ni pamoja na Aunty Sadaka,Hilda Kisoka, Dr. Rose Malissa,Advocate Salome na Edna Shoo.