Yanga SC imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya timu ngumu kwao kihistoria, Lipuli FC ya Iringa katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Yanga SC nayofundishwa na Mbelgiji Luc Aymael anayesaidiwa na mzawa, Charles Boniface Mkwasa, kocha wa Fiziki, Riedoh Berdien kutoka Afrika Kusini na kipa wa zamani wa klabu, Manyika Peter anayewanoa walinda milango wa timu hiyo – inafikisha pointi 34 baada ya kucheza mechi 17 na kupanda nafasi ya tatu.
Sasa inazidiwa pointi nne na Azam FC na pointi 16 na vinara na mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo kwa pamoja wamecheza mechi mbili mbili zaidi.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abubakar Mturo wa Mtwara aliyesaidiwa na Makame Mdogo na Joseph Pombe wote wa Shinyanga, hadi mapumziko Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Kiungo Mapinduzi Balama alianza kuwafungia Yanga SC dakika ya 14 kwa kichwa cha mkizi akimalizia krosi ya beki wa kulia, Juma Abdul.
Kiungo Mghana, Bernard Morrison akatanua uongozi wa Yanga kwa kufunga bao la pili dakika ya 33 kwa shuti la mguu wa kulia akimalizia krosi ya Juma Abdul pia.
Yanga SC ingeweza kuondoka na mabao zaidi kipindi cha kwanza kama mshambuliaji wake mpya, Yikpe Gilsain kutoka Ivory Coast angetumia vyema nafasi alizopata.
Kipindi cha pili mambo yakabadilika na Lipuli wakauteka mchezo na kuliweka kwenye musukosuko lango la Yanga SC ambayo kasi yake ilipungua kabisa.
Wachezaji wa Lipuli walimfuata kumlalamikia mshika kibendera namba moja, Makame Mdogo dakika ya 55 baada ya kuamuru mpira ulioonekana kama umeekolewa na ndani na kipa wa Yanga, Metacha Mnata upigwe kona.
Lipuli FC wakafanikiwa kupata bao la kufutia machozi dakika ya 58 baada ya shuti la mpira wa adhabu liliupita ukuta wa Yanga na kipa wao Mnata.
Lipuli wakaendelea kulitia misukosuko lango la Yanga, huku wakizuia vizuri na kutibua mipango yote ya wapinzani wao.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Juma Abdul, Jaffar Mohamed, Lamine Moro, Said Juma ‘Makapu’, Papy Kabamba Tshishimbi, Ditram Nchimbi/Deus Kaseke dk71, Haruna Niyonzima/Ally Mtoni dk81, Yikpe Gislain/David Moringa ‘Falcao’ dk61, Balama Mapinduzi na Bernard Morrison.
Lipuli FC; Deogratius Munishi ‘Dida’, David Kameta, Paul Ngalema, Peter Mwangosi, David Mwasa, Novaty Lufunga, Said Mussa/Zubery Ada dk70, Freddy Tangalu, Paul Nonga, Daruweshi Saliboko na Keneth Masumbuko.
CHANZO- BINZUBEIRY BLOG