VIGOGO, Yanga SC wamelazimishwa sare ya pili mfululizo nyumbani baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana na Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara usiku huu Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Sare hiyo inawaongezea pointi moja Yanga SC na kufikisha pointi 39 katika mchezo wake wa 20 wa msimu, ikibaki nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC yenye pointi 44 na mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 56 baada ya wote kucheza mechi 22.
Hiyo inakuwa sare ya pili mfululizo nyumbani baada ya Yanga kulazimishwa sare nyingine ya 1-1 na Mbeya City kwenye mchezo uliopita hapa hapa Dar es Salaam.
Hata hivyo, Yanga itabidi wajilaumu wenyewe kwa kupoteza nafasi nzuri ya kupata bao dakika ya 73 leo baada ya kiungo wake Mghana, Bernard Morrison penalti kufuatia kupiga juu ya lango.
Penalti hiyo ilitolewa baada ya yeye mwenyewe, Morrison kuangushwa kwenye boksi na kipa wa Tanzania Prisons, Jeremiah Kisubi, ingawa refa Hance Mabena ilibidi akajiridhishe kwa msaidizi wake namba moja, Leonard Mkumbo kabla ya kutenga tuta.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Farouk Shikhalo, Juma Abdul, Adeyoum Ahmed, Lamine Moro, Ally Mtoni ‘Sonso’, Papy Kabamba Tshshmbi, Mapinduzi Balama, Mohammed Issa ‘Banka’/ Mrisho Ngassa dk77, Yikpe Gislain/ David Molinga dk60, Tariq Seif/Deus Kaseke dk63 na Bernard Morrison.
Tanzania Prisons; Jeremiah Kisubi, Michael Ismail, Laurian Mpalile, Vedastus Mwihambi, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhili, Cleophace Mkandala/ Ismail Aziz dk86, Ezekia Mwashilindi, Paul Peter, Jeremiah Juma/ Lambert Sabiyanka dk58 na Adili Buha.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Nahodha John Rapahel Bocco liliipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Lipuli FC 1-0 Uwanja wa Samora mjini Iringa.
Ruvu Shooting ikaichapa 1-0 Mbeya City bao pekee la Fully Maganga dakika ya 50 Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Biashara United pia ikaibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Alliance bao pekee la Okorie James dakika ya 45 na ushei Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara.
Ndanda FC ikaibuka na ushindi wa ugenini wa 1-0 dhidi ya Singida United, bao pekee la Vitalisy Mayanga dakika ya 80 Uwanja wa Liti, Singida.
JKT Tanzania ikaibuka na ushindi wa ugenini wa 1-0 pia dhidi ya Mtibwa Sugar, bao pekee la Danny Lyanga dakika ya 33 kwa penalti.
Mwadui FC ikatoka nyuma na kupata sare ya ya 1-1 nyumbani na Namungo FC Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.
Namungo ilitangulia kwa bao la Nzigamasabo Steve dakika ya nane kabla ya Raphael Aloba kuisawazishia Mwadui dakika ya 49.
Nayo Kagera Sugar ikaibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Mbao FC, mabao yake yakifungwa na Geoffrey Mwashiuya dakika ya nane na Yusuph Mhilu dakika ya 31 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Polisi Tanzania ikaibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya wenyeji, Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, mabao yake yakifungwa na Marcel Kaheza dakika ya 10, Matheo Anthony dakika ya 39 na Baraka Majogoro dakika ya 87 – na ya wenyeji yakifungwa na Abdul Hillary dakika ya 80 na Ally Ramadhani dakika ya 83.
CHANZO - BINZUBEIRY BLOG
Social Plugin