Mahakama ya juu ya Pietermaritzburg nchini Afrika Kusini imetoa hati ya kukamatwa kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma baada ya kushindwa kufika mahakamani kukabiliana na mashtaka kuhusu rushwa dhidi yake.
Hati hiyo itafanya kazi ikiwa atashindwa kuhudhuria kesi yake itakayoanza mwezi Mei. Bwana Zuma anakabiliwa na makosa 16 ya kughushi, rushwa , ulaghai na utakatishaji fedha ukihusisha biashara ya silaha ya thamani ya mabilioni ya dola iliyofanywa tangu miaka ya 1990.
Rais huyo wa zamani amefanikiwa kukwepa shutuma za rushwa dhidi yake kwa zaidi ya miaka 10. Lakini leo, sheria haikuwa upande wake.
Hati ya kukamatwa kwake imetolewa baada ya kushindwa kufika mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi yake. Jopo la wanasheria wake waliwasilisha nyaraka wakisema kuwa mteja wao alikuwa mgonjwa na amekuwa akipatiwa matibabu nje ya Afrika Kusini tangu mwezi uliopita.
Jaji Dhaya Pillay alihoji maelezo yaliyo kwenye nyaraka za matibabu za Zuma zilizowasilishwa na mawakili wake mahakamani. Lakini rais huyo wa zamani atakamatwa ikiwa atashindwa kufika mahakamani tarehe 6 mwezi Mei kesi yake itakapoanza rasmi.
Chanzo- BBC