Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ASKOFU GWAJIMA AHOJIWA NA JESHI LA POLISI KWA TUHUMA ZA KUHAMASISHA UKABILA NCHINI


Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemuhoji Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, JOSEPHAT GWAJIMA kwa tuhuma za kusambaza kipeperushi na sauti kwa lugha ya kisukuma zenye lengo la kuhamasisha watu kuunda kikundi cha kikabila nchini. 

Kipeperushi hicho chenye picha ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimesambaa kwenye mitandao ya kijamii kikiwa na maandishi yanayosomeka kwa lugha ya kisukuma.

Sambamba na kipeperushi hicho, askofu Gwajima pia ametoa ujumbe wa sauti wenye ujumbe wa kumpongeza mhe. 

Rais na kuhamasisha wasukuma kurejesha utamaduni wao wa zamani wa kutumia lugha yao, kusaidiana katika shida na raha na kuwataka wasukuma kuunda vikundi kwenye mitandao ya kijamii vya watu elfu mbili (2000) kwa lengo la kufuatilia watu wanaomtukana mhe. Rais na kuwashughulikia.

Katika ujumbe huo wa sauti askofu Gwajima pia amewataka wasukuma matajiri kuungana kwa pamoja kwa lengo la kuwasaidia wasukuma masikini ili kuondoa dhana ya kwamba wasukuma ni masikini na ni washamba.

Kufuatia jumbe hizo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemuhoji askofu Gwajima kutokana na jumbe hizo kuonekana kuhamasisha vitendo vya kikabila jambo ambalo linaweza kuwagawa watanzania na kupelekea kuvunjika kwa amani na mshikamano wa nchi utakaotokana na uwepo wa matabaka ya kikabila.

Baada ya mahojiano hayo, Jeshi la Polisi kanda Maalum ya Dar es Salaam limemuonya askofu Gwajima kuacha mara moja vitendo vya kuligawa taifa kwa kutumia vigezo vya ukabila na kutoa onyo kwa wote wenye nia ya kutaka kuligawa taifa kwa njia ya ukabila, udini au ukanda.

Jeshi la Polisi halitamuonea muhali mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya aina hiyo na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linatoa wito kwa wananchi kuendeleza umoja na mshikamano uliopo nchini bila kujali dini, kabila wala rangi ya mtu kama ambavyo baba wa taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere alivyopinga vitendo vya kibaguzi na kutuunganisha kuwa wamoja kwa lugha ya Kiswahili. 

CAMILLIUS M. WAMBURA – SACP
KAIMU KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAM.
03/03/2020


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com