Jeshi la polisi mkoani Kagera linamshikilia Frank Kafuba mkazi wa Kayanga wilayani Karagwe mkoani Kagera kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mwendesha bodaboda mwenzake Mugisha Theonest mwenye umri wa miaka 52, aliyefariki baada ya kushambuliwa na bodaboda wenzake.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera Revocatus Malimi, amesema kuwa bodaboda aliyeuawa, akiwa na mwenzake aitwaye Erick Cosmas walipeleka abiria eneo la ranchi ya Taifa ya Kagoma na wakati wakirejea Kayanga, walikuta abiria barabarani aliyekuwa akimsubiria dereva bodaboda aliyemuita, lakini kwa kuwa alichelewa abiria huyo aliamua kupanda bodaboda ya Mugisha.
Kamanda Malimi amesema kuwa, wakiwa wanaendelea na safari njiani walikutana na bodaboda aliyekuwa amepigiwa simu akamtaka mteja wake amlipe gharama za mafuta maana alimuita, lakini abiria huyo hakukubali na kuwa ndipo bodaboda huyo alipiga simu kwa bodaboda wa kijiwe chake, akadai kuna watu wanataka kumpora pikipiki.
Amesema bodaboda hao walikwenda kutoa msaada kwa mwenzao na kuanza kumshambulia Mugisha na kumjeruhi vibaya, na kuwa siku hiyo ya Machi 04 alipelekwa Hospitali teule ya Wilaya ya Karagwe ya Nyakahanga, ambapo alifariki wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa Kamanda Malimi, jeshi hilo linaendelea kuwasaka Bodaboda wengine walioshirikiana na Frank Kafuba kumuua bodaboda mwenzao wakimsingizia ni mwizi wa pikipiki wakati waligombania abiria.
Social Plugin