Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BITEKO ASEMA IMETOSHA KUHUSU MCHUCHUMA NA LIGANGA


Na Issa Mtuwa – Ludewa
Serikali kupitia Waziri wa Madini Doto Biteko amesema, serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano kuhusu miradi ya mchuchuma na Liganga ili iweze kuanza. Ameongeza kuwa mradi wa mchuchuma na Liganga ni miradi ya miaka mingi lakini haina tija na ndio maana serikali ya awamu ya tano iliamua kufuatilia kuhusu mikataba ya miradi hiyo ili kuona kama ina tija kwa taifa wakiwemo watu wa Ludewa. 


Akizungumza jana tarehe 15 Machi, 2020 wakati wa mkutano na wananchi wa kijiji cha Mundindi wilayani Ludewa,Waziri wa Madini Doto Biteko amesema, pamoja na kuchelewa kuanza kwa miradi ya Mchuchuma na Liganga, kuna manufa makubwa kwa wananchi na taifa kuliko miradi hiyo ingeanza kabla kufanyika kwa majadiliano yanayoendelea.  


“Ndugu zangu niseme stori za Mchuchuma na Liganga imetosha. Nafahamu mnamahitaji makubwa kuona hii miradi ianze, hata mimi nikiwa mdogo nimeshasikia sana kuhusu miradi ya Mchuchuma na Liganga, serikali tunayo sabau ya kuangalia maslai yenu na taifa. naomba niwaambie, serikali yenu ipo kwa ajili yenu, naomba kuweni na  subira” alisema Biteko. 


Biteko ameongeza kuwa serikali iligundua mambo mengi yasiyo na tija kuhusu mikataba ya miradi hii ndio maana tuliamua kufanya majadiliano ilikuona namna gani serikali itakavyonufaika. Mmekuwa wapole, watulivu na wasikivu ni jambo zuri sana, niwaombe endeleni kuwa wavumilivu  viongozi wenu wa mkoa na wilaya, mbunge na diwani wenu wamekuwa na kilio kama chenu ndio maana niliamua nije niweze kuzungumza na ninyi.  


Biteko amesema, hakuna mwananchi yeyote atakae punjwa kuhusu fidia yake, serikali italisimamia suala hilo kwa uzito mkubwa. 


“Nawaomba. kuweni na imani na serikali yenu, nitasimamia kama nilivyosimamia fidia za wananchi wa  Nyamongo wilayani Tarime dhidi ya Mgodi wa North Mara waliokuwa wanahitaji maeneo ya wananchi.  


Ndugu zangu ninachotaka kila jamii inufaike na mali zilizopewa na mungu. Ludewa najua mnataka kunufaika na miradi ya Mchuchuma na Liganga kama ambavyo Geita wananufaika na Dhahabu, Shinyanga wananufaika na Almasi,  Songea wananufaika na Makaa ya Mawe, Arusha wananufaika na Tanzanite na Tanga wananufaika kuhusu vipepeo vya kila aina.” aliongeza Biteko. 


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka amemshukuru Waziri kwa kutimiza ahadi yake ya kuja Njombe kwa ajili ya ziara hii na kutembelea maeneo mbalimbali ya maeneo ya sekta ya madini na kuzungumza na wananchi hasa wa Ludewa ambao wanakilio kikubwa kutokana na kuchelewa kwa miradi ya Mchuchuma na Liganga. 


Diwani wa Kata ya Mundindi, Wise Mgina, amemweleza Waziri kuwa watu wa Ludewa wanapenda kuona miradi hiyo ikianza kwa kuwa ni miradi ya muda mrefu na wananchi wake wanashindwa kuendeleza ardhi hiyo kutokana zuio hivyo wanaiomba serikali miradi hiyo ianze ili iwanufaishe wananchi wake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com