Na Fortune Francis, Mwananchi
Rais wa Tanzania, John Magufuli amemlipia Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa faini ya Sh38 milioni kati ya Sh40 milioni anazotakiwa kulipa mbunge huyo ili atoke jela.
Msigwa ni kati ya viongozi wanane wa Chadema ambao pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji Jumanne Machi 10, 2020 walihukumiwa kulipa faini ya Sh350 milioni au kwenda jela miezi mitano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliyokuwa yanawakabili.
Washtakiwa hao wakiongozwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walilazimika kwenda jela baada ya kushindwa kukamilisha taratibu za kulipa faini hiyo waliyohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Baada ya hukumu hiyo iliyosomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Chadema walianza kuchangishana fedha kwa ajili ya kuwalipia faini viongozi wake hao.
Hadi leo saa 9 alasiri, wabunge waliolipiwa faini na kutoka jela ni ni Ester Bulaya (Bunda), Esther Matiko (Tarime Mjini) na Halima Mdee (Kawe).
Ambao bado wapo katika gereza la Segerea ni Mbowe, John Heche (Tarime Vijijini), John Mnyika (Kibamba), naibu katibu mkuu wa chama hicho-Zanzibar, Salum Mwalimu na Mchungaji Msigwa.
CHANZO- MWANANCHI
Social Plugin