Na Amiri kilagalila,Njombe
Kutokana na tishio la ugonjwa wa Corona (COVID 19) unaeoendelea kuenea nchi nyingi Duniani huku Tanzania ikifikia wagonjwa 6 mpaka sasa kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waziri wa afya maendeleo ya jamii, jinsia na watoto Ummy Mwalimu.
Katibu wa chama cha walimu CWT mkoa wa Njombe Mwalimu Fraten Kwaison amesema kutokana na agizo la serikali kuwataka watanzania kutokujihusisha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima pamoja na njia nyingine zinazowezesha kujikinga na maambukizi ya virusi vya COVID 19,chama hicho kimesitisha uchaguzi wa viongozi ngazi ya wilaya ambao ulitarajiwa kufanyika kuanzia machi 21-28 2020 kwa kuwa unakutanisha watu Zaidi ya 100.
“Kwa ngazi ya wilaya uchaguzi wetu ungefanyika tarehe 21 mpaka 28 ya mwezi huu wa tatu sasa baada ya tangazo kutoka tumesitisha,na tumesitisha kwasababu mikutano hii inayofanyika ni mikubwa na inakwenda takribani watu 100 na kuendelea,kwa hiyo kwa tangazo lililotolewa na serikali ilikuwa ni muhimu sana kusitisha”alisema Kwaison
Aidha Kwaison amesema chaguzi nyingine upande wa shule mahali pa kazi upande wa shule za misingi,sekondari,vyuo vya ualimu na vyuo vya maendeleo ya wananchi uchaguzi umekwisha fanyika lakini kwa ngazi ya wilaya umeahirishwa kutokana na kutii agizo la serikali.
Vile vile amesema kwa upande wa maandalizi ya sherehe za mei mosi chama kinaendelea kukusanya michango kwa wadau kwa kuwa watu wamekwishaainishwa na sherehe hizo zitafanyika kutokana na muelekeo wa serikali.
“Kwasababu watu walishaainishwa kazi iliyobakia ni kuwapelekea barua kwenye ofisi zao na manyumbani kwao kwasababu tarehe ambayo tulikusudia michango kukamilika ni tarehe 17 mwezi wa 4 kila mmoja awe amejua cha kuchangia,kwa hiyo utekelezaji huo unaendelea kwa upande wa Mei mosi,na serikali ikitoa muelekeo na nini cha kufanya basi sherehe itaendelea kufanyika ila hatuwezi kukaa tukaacha kukusanya hiyo michango wakisema hitafanyika hiyo ni kitu kingine”alisema tena Fraten Kwaison
Katika hatua nyingine Bwana Kwaison ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwalinda watoto kwa kuwa shule zimefungwa kwa dharula na sasa wapo mikononi mwao hivyo ni wajibu wa wazazi na wanafunzi kujilinda kwa kipindi hiki cha kufungwa shule kwa dharula kutokana na ugonjwa wa COVID 19.
“Kwa sasa watoto wako mazingira huru na wamekwenda kwa jamii,ninaomba wazazi wasiwaache watoto huru ila wawadhibiti vizuri ili warudi shuleni wakiwa salama na ukizingatia mitaani kuna mambo mengi,lakini kubwa kwenye hili la CORONA tunaendelea kukumbasha mpaka huku majumbani ni lazima tujikinge kweli kweli”alisema tena Kwaison.
Serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania imetoa utaratibu mbali mbali ikiwemo kufunga shule za awali mpaka vyuo vikuu na vya kati,pamoja na kuzuia mikusanyiko isiyo kuwa ya lazima ili kuzuia na kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona (COVID 19) huku mpaka serikali ikiwa imetangaza takribani watu 6 kukumbwa na virusi hivyo.
Social Plugin