Na Jackline Lolah Minja - Malunde 1 blog
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa leo Jumatano Machi 4,2020 ametembelea na kukagua Ujenzi wa Daraja la Kiyegea lililopo wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro (barabara ya Morogoro - Dodoma) na kuwataka wananchi na wasafiri kuwa wavumilivu wakati huu ambapo utengenezwaji wa daraja hilo lililokatika unaendelea.
Waziri Mkuu, amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi pamoja na wakandarasi wa mkoa wa Dodoma na Morogoro kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kuwezesha ujenzi wa daraja hilo kumalizika haraka.
"Naagiza Jeshi la Wananchi Tanzania pamoja na wakandarasi wote wa Dodoma na Morogoro kuja hapa na kufanya kazi usiku na mchana ili hadi kesho barabara ianze kupitisha magari hata madogo na itafutwe njia mbadala kwa ajili ya magari makubwa kupita",amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Aidha amewataka wakandarasi wote kuhakikisha wanatembelea mara kwa mara maeneo yote ya madaraja hasa kipindi hiki cha mvua zinaoendelea kunyesha ili kuepuka madhara kama haya kujitokeza.
Daraja hilo lilikatika kwa kusombwa na maji juzi Machi 2,2020 saa 9 alasiri kufuatia mvua zinazoendelea.
Malunde1 blog imeshuhudia msururu wa magari katika eneo hilo huku mamia ya watu wakihaha huku na kule kutafuta mahitaji mbalimbali.
Wakizungumza na Malunde 1 blog, baadhi ya abiria na madereva waliokwama kuendelea na safari wanasema wanauziwa chakula kwa bei ya juu kuliko awali.
Inaelezwa kuwa hivi sasa sahani moja ya chakula inauzwa Sh3,500 hadi 4,500 badala ya Sh2,000, chupa ya maji na soda sasa ni Shilingi 1,000/= hadi 1,500/= kutoka Sh500 hadi Shilingi 700 huku ikidaiwa kuwa katika eneo hilo linakabiliwa na shida ni huduma ya choo na eneo la kuoga.
Baadhi ya madereva waliokwama hapo wanasema hawaweze kupitia Iringa kwa kuwa hawana mafuta ya kutosha kupita huko.
Jana Jumanne Machi 3,2020 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema hadi usiku wa kuamkia leo Jumatano Machi 4,2020 magari yatakuwa yanapita eneo hilo jambo ambalo limekuwa tofauti.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza wakati akikagua Ujenzi wa Daraja lililokatika barabara kuu ya Morogoro - Dodoma leo Jumatano Machi 4,2020.
Muonekano wa ujenzi wa ujenzi wa Daraja hilo leo mchana.
Social Plugin