Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amesema kwamba ndani ya Mkoa huo amebainika kuwepo kwa mgonjwa mmoja wa Corona na kwamba hoteli ambayo amekutwa mgonjwa huyo imefungwa na hivyo hakuna anayeingia wala anayetoka.
Akizungumza Machi 16 mwaka 2020 , Mkuu wa Mkoa wa Arusha Gambo amesema kama ambavyo ameeleza Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ni kweli wamepata mgonjwa mmoja wa Corona na kwa mujibu wa taarifa huyo mgonjwa alishuka jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro kwa kutumia ndege ya Rwanda Air.
Amesema kuwa mgonjwa huyo alifikia kwenye hoteli inayofahamika kwa jina la Temi Valle Hoteli ya jijini Arusha na kwamba baadae alienda hospitali Mount Meru kwa ajili ya kuchukuliwa sampuli na kisha kupelekwa Dar es Salaam ambako kuna maabara ya kupima sampuli za Corona na kubainika ni kweli ana Corona.
"Na tulichokifanya sisi kama Serikali za ngazi ya Mkoa kwanza ile hoteli ambayo mgonjwa alifikia tumeifungia na hakuna mtu kuingia wala kutoka kati ya wafanyakazi na wahusika wote waliokuwa wanakaa kwenye hoteli hiyo, ,hatua ambayo tumechukua ni kuchukua sampuli kwa ajili ya watu wote katika hoteli hiyo kubaini kama kuna wengine walioambukizwa.
"Lakini hatua ya tatu ambayo tumechukua kama Mkoa ni kutenga eneo maalum iwapo atapatikana mgonjwa yoyote ambaye atapelekwa kwenye eneo hilo kwa ajili ya hatua nyingine za matibabu.Pia tunamfuatilia dereva taksi ambaye alimpakia mgonjwa Corona pamoja na familia yake ili naye achunguzwe kama hajapata maambukizi, "amesema Gambo.
Amewatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Arusha waendelee kuwa watulivu kwani Serikali imechukua hatua stahiki katika kukabiliana na ugonjwa huo huku akieleza namna ambavyo wamefuatilia mtandao wote wa watu ambao kwa namna moja au nyingine walimpokea mgonjwa huyo wanapatikana na kisha kupimwa, lengo ni kuhakikisha Mkoa huo maambukizi hayasambai.
Social Plugin