Mchekeshaji maarufu nchini Tanzania, Idris Sultani (27) na wenzake wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kujibu shtaka moja la kuchapisha maudhui mtandaoni bila kuwa na leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Sultani(27) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Beach na wenzake wamesomewa shtaka lao, leo Ijumaa Machi 20, 2020, mahakamani hapo.
Mbali na Sultani, washtakiwa wengine ni mfanyabiashara Doctor Ulimwengu (28) mkazi wa Mbezi Beach na Isihaka Mwinyimvua (22) ambaye ni msanii na mkazi wa Gongolamboto.
Washtakiwa hao wamesomea shtaka lao na wakili wa Serikali, Batilda Mushi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Wakili Mushi alidai washtakiwa wote wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 60/2020.
Amedai washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Machi 8, 2016 na Machi 13, 2020 katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, kwa kutumia online Tv inayojulikana kwa jina la Loko Motion, walichapisha maudhui katika mtandao huo bila ya kuwa na kibali kutoka TCRA, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka hilo, walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hakimu Shaidi, alitoa masharti ya dhamana ambayo, kila mshtakiwa alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh 8milioni.
Pia, mdhamini huyo anatakiwa kuwa na barua inayotambulika kisheria na kitambulisho cha Taifa.
Washtakiwa wote wametimiza masharti ya dhamana na hakimu Shaidi, ameahirisha kesi hiyo hadi April 21, 2020 itakapotajwa.
Social Plugin