Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU inapenda kuufahamisha umma kwamba, watumishi wake wawili akiwemo Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, wamesimamishwa kazi kuanzia Machi 20, 2020 ili kupisha uchunguzi dhidi yao. Hatua hii imefikiwa leo baada ya watumishi hao:
(i)Christopher Mariba – Aliyekuwa Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga na
(ii) Hilton Njau – Afisa Uchunguzi Mkuu kutoka ofisi ya TAKUKURU mkoa wa Tanga, kuhusishwa na tuhuma za kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa mmoja wa watuhumiwa waliokuwa wakichunguzwa na TAKUKURU.
Kosa hili ni kinyume na Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kama ambavyo nimekuwa nikiuleza umma mara kwa mara, chombo hiki ndicho chenye dhamana ya kuongoza mapambano dhidi ya rushwa nchini – jukumu ambalo tumepewa kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007.
Kwa msingi huo, watumishi wa TAKUKURU wanapaswa kuwa na uadilifu na weledi wa hali ya juu wakati wote wanapotekeleza majukumu haya nyeti kwa mustakabali wa maendeo na ustawi wa Taifa letu.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Ili kuhakikisha kuwa chombo hiki hakichafuliwi, ipo SERA ya ndani ya chombo hiki YA KUTOMVUMILIA MTUMISHI YEYOTE ANAYETUHUMIWA KUJIHUSISHA NA VITENDO VYA RUSHWA. Hivyo basi, kwa msingi huo, watumishi hawa wamesimamishwa kazi kuanzia leo Machi 20, 2020 ili kupisha uchunguzi dhidi yao na uchunguzi huo utakapokamilika hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa.
Wakati uchunguzi huu ukiendelea, nimemteua Dkt Sharifa Bungala kukaimu nafasi ya Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Tanga kuanzia Machi 20, 2020.
BRIG. JEN JOHN MBUNGO (ndc)
KAIMU MKURUGENZI MKUU – TAKUKURU
Social Plugin