Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Biswalo Mganga, amesema bado ofisi yake na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), wanalifanyia kazi sakata la tuhuma za aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola na aliyekuwa Kamishna wa Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye.
Alisema taasisi hizo mbili zina utaratibu wa kufanyakazi na kwamba hakuna jambo la kificho, kila kitu kitakapokuwa tayari umma utafahamishwa kupitia vyombo vya habari.
Akizungumza na waandishi habari ofisini kwake alisema kuna utaratibu wa utendaji wa kazi zao hivyo suala hilo likiiva litawekwa hadharani.
"Kwa sasa sina majibu siwezi kusema jalada la Kangi na Andengenye kama limefika ofisini kwangu au la, sina utaratibu wa kutoa taarifa nusu nusu, muda ukifika nitawaita niwaeleze kinachoendelea," alisema DPP.
Lugola alivuliwa madaraka baada ya Rais John Magufuli kuonyesha kusikitishwa na utendaji wa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani hasa utiaji saini wa mkataba wa mradi wa thamani ya Euro milioni 408.
Aliamua kutengua uteuzi wa Lugola wa Uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na nafasi yake kuchukuliwa na George Simbachawene na kisha kuagiza TAKUKURU Wamchunguze na wachukue hatua.
Social Plugin