Na Dinna Maningo - Tarime
Ni saa tisa alasiri nawasili nyumbani kwa Prisca Kibasa mwenye umri wa miaka (56) ambaye ni Mwenyekiti wa mtaa wa Kibasa kata ya Sabasaba wilaya yaTarime mkoani Mara kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ananikaribisha huku usoni kwake akionekana mtu mwenye furaha.Lengo la kufika kwake nikutaka kufahamu ni kwa namna gani anawatumikia wananchi ikiwa ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa mtaa.
Licha ya kwamba baadhi ya wanawake hawajitokezi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwa uoga waliojijengea kutokana na dhana zilizopo ndani ya jamii kuwa mwanamke hana haki kuzungumza mbele ya watu au kuwaongoza wanaume lakini hali hiyo ni tofauti kwa mama Kibasa.
Mama Kibasa ambaye amekuwa kiongozi ngazi ya kitongoji na Mtaa tangu mwaka 2004 hadi sasa ni kiongozi akihakikisha anaimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi na mali zao na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Je Kwanini Mwenyekiti huyo anaitwa Prisca Kibasa na mtaa nao unaitwa Kibasa?
"Wakati tunagawa mitaa nilikuwa ni Mwenyekiti nikasema kwanini niite majina mengine nikaita jina langu hata nije kukumbukwa kwa hilo na nilipoita na wengine nao wakajiitia majina yao kama mtaa wa Nyangai,Chomete,na mtaa wa Nyarusai kwa hiyo ndiyo ujue kuwa mwanamke akiamua kufanya jambo inawezekana na wengine wakaiga kutoka kwako",anasema Kibasa.
Kibasa anaeleza historia yake ya uongozi ambapo anasema kuwa amekuwa mwenyekiti wa Kitongoji cha Serengeti kwa awamu mbili mfululizo tangu mwaka 2004 hadi 2014.
"Wakati huo ilikuwa ni halmashauri moja ya wilaya mimi nilikuwa ndiyo mwanamke peke yangu niliyechaguliwa hadi nilikuwa najishangaa nikisimama kuzungumza mbele ya wanaume nilikuwa naona aibu, lakini baadae nilizoea nikajiamini kwanini nijishushe nawakati nimegombea sawa na wanaume" anasema Kibasa.
Kibasa anaeleza kuwa licha ya kuwa kiongozi mwanamke pekee wananchi walimpa ushirikiano kutokana na ujasiri wake na kujituma uliofanikisha kuleta maendeleo kutokana na ushawishi baina yake na wananchi.
"Mimi si Mkurya kabila langu ni mrangi wa Kondoa niliolewa na mkurya pamoja nakwamba mimi ni mkabila tena musagane mwanamke ambaye sikukeketwa bado wananchi waliniona nafaa wakanichagua. Kitongoji chetu kilikuwa na wananchi 490 walinichagua kwa sababu mimi sipendi rushwa na sina ubaguzi huduma yangu wanahifurahia",anasema.
Anaongeza"Nilipokuwa mwenyekiti wa kitongoji tulifanikiwa kujenga madarasa shule ya msingi Sabasaba,darasa moja shule za Sekondari Nyamisangura,Rebu na Nkende, kuimarisha ulinzi shirikishi na shughuli zingine za kimaendeleo".
Akizungumzia suala la ulinzi shirikishi anasema kuwa pamoja na yeye kuwa kiongozi mwanamke hakusita kutembea usiku akiwa ameambatana na wanaume kuhakikisha wanazunguka maeneo yote ya kitongoji kuimarisha ulinzi.
Anasema kuwa wakati wa zamu ya ulinzi aliwaandaa wananchi na kuwapanga kwa makundi kisha kupita kwenye maeneo ya giza na vichochoro vyote jambo ambalo lilifanikisha baadhi ya wahalifu kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
"Tulikuwa tunaanza ulinzi saa sita usiku nachagua watu kwa zamu nilivaa mavazi yangu Suruali,kofia na jaketi kisha tunaenda kulinda,lazima na mimi Mwenyekiti niende maana ukiacha waende wenyewe wapo baadhi ya wananchi si wazuri watatumia muda huo kufanya uhalifu kama kuwaibia simu wapita njia,kabla ya kuanza ulinzi tunakutana nyumbani kwangu nawapanga makundi matatu yenye watu sita tunaondoka kila kundi linaenda sehemu yake kufanya ulinzi.
"Tulikuwa tunalinda hadi saa kumi kisha tunakutana mahali ambapo tumepanga kukutana ili kuona kama tuko wote, kwakweli tulifanikiwa sana maana tulikuwa tunawapata wezi, maeneo mengine tulikuta vitu vilivyoibwa vimetunzwa ,wakati wa ulinzi tuliwapa Polisi Taarifa na walifika kubeba na kuwakamata wezi, kabla ya kuwakabidhi Polisi tulikuwa tunawapa kwanza kichapo",anasema Kibasa.
Mbali na kuwa Mwenyekiti wa Kitongoji mwaka 2019 katika uchaguzi wa Serikali za mitaa Mama Kibasa aliibuka tena na kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa mtaa wa Kibasa na alifanikiwa kupita katika kura za maoni kupitia chama cha CCM dhidi ya wapinzani wake.
"Nilishindana na wanaume wawili mwanamke nilikuwa mimi peke yangu na nikawashinda na sasa mimi ni mwenyekiti wa mtaa japo napata changamoto kuwa hatukuchaguliwa na wananchi lakini hainikatishi tamaa mimi ndiyo mwenyekiti wao bahati nzuri wengi wananikubali".
"Kuna mwananchi mmoja waligombana nikamwita kwa barua alikataa kuja akasema hanitambui kwakuwa ninajiamini nikamwambia sasa utanitambua kuwa mimi ni mwenyekiti na kufikisha ngazi za juu alivyoona nimekuwa mkali alikuja kuomba radhi kwa kuwa alikiri kosa nikamsamehe nilitaka nimwonyeshe kuwa hata mwanamke ana uwezo wa kujisimamia",anasema Kibasa.
Mahende Kangoye mkazi wa mtaa wa Kibasa anasema Mwenyekiti huyo anafaa kuongoza kwa kuwa ni mtu anayejali watu na kwamba hakuna changamoto inayotokea akashindwa kuitatua,anasisitiza kuwa kadri siku zinavyokwenda mila kandamizi zinapungua.
Kangoye anasema kuwa baadhi ya wanawake ni waoga kusimama mbele za watu hali inayosababisha wasigombee,anasema usipokuwa jasiri huwezi kuongea au kushauri jambo kwenye mikutano.
Anaongeza kwamba mila ya Kabila la Wakurya mwanamke hawezi kufanya jambo bila ruhusa ya mme wake na wengine ukataliwa na ukijichukulia maamuzi yao hufukuzwa nyumbani hali inayosababisha wengine kuacha kugombea.
"Wapo baadhi ya wanaume wakiona mwanamke anaongea jukwaani wanasema huyu mwanamke ni shida nyumbani mara atakuwa ana sauti nyumbani, ukienda kwenye vikao ukachelewa anadhani ulikuwa kwa wanaume",anasema.
Anaongeza" ni vyema wanaume waelimishwe watambue kuwa hata mwanamke anaweza kuongoza na kuna wanawake wana uwezo lakini niwaoga anajiuliza kuwa nikipata uongozi je nitahimili mikikimikiki ya vijana, nitaweza kweli anaamua kuacha" anasema Kangoye.
Katibu wa Umoja wa Wanawake Chama cha Mapinduzi (UWT) wilaya ya Tarime Sauda Kashombo anasema kuwa kuna haja ya elimu kuendelea kutolewa ili kuwapa fursa kugombea na kwamba wasiwe na hofu kwani uongozi si nguvu bali ni akili.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Tarime Mkaruka kura anasema kuwa baadhi ya wanawake hawajiamini kuwa wana uwezo wa kugombea na wanaume na kwamba Chama cha Mapinduzi hutoa kipaumbele kwa wanawake lakini baadhi yao wanashindwa baada ya kutopigiwa kura wakati wa kura za maoni na kwenye uchaguzi.
Lilian Liund ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) anasema kuwa ushindi wa wanawake kwenye chaguzi hutegemea uamuzi wa wapiga kura,wanawake kwa wanaume, na kwamba wanawake ndiyo ujitokeza kwa wingi kupiga kura ikilinganishwa na wanaume.
Liund anatoa rai kwa wanawake na wanaume kuwapigia kura wanawake wenye uwezo na wenye kubeba ajenda ya ukombozi wa mwanamke,kuhakikisha wanahamasisha wanawake wenye uwezo wanajitokeza kugombea,Kushawishi vyama kuteua wanawake,kuwapa moyo wanawake waliojitokeza kuwania viti vya uchaguzi na kuwapigia kura.
Social Plugin