Asteria Muhozya na Tito Mselem, Dodoma
Wizara ya Madini imesema hakuna majadiliano yoyote yanayoendelea kati ya Serikali na Kampuni ya TanzaniteOne na badala yake Leseni ya Kitalu C iliyokuwa inamilikiwa na kampuni hiyo kwa ubia na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imefutwa kwa mujibu wa Sheria na tayari eneo hilo limerudishwa Serikalini na hakuna mwekezaji mpya.
Kauli kuhusu suala hilo zilitolewa Machi 11, 2020 kwa nyakati tofauti na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Katibu Mkuu wa Madini Prof. Simon Msanjila na Mkurugenzi wa Leseni Tume ya Madini Mhandisi Yahaya Samamba wakati wa kikao kazi kati ya Wizara na Kamati ya Eneo lililodhibitiwa la Mirerani (Mirerani Controlled Area) kilichofanyika Jijini Dodoma.
Mbali na Kamati hiyo, kikao hicho pia kilihudhuriwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga, Mkuu wa Wilaya ya Simajiro Mhandisi Zephania Chaula ambaye ni Mwenyekiti wa Eneo lililodhibitiwa la Mirerani, pamoja na Uongozi wa Tume ya Madini.
Waziri Biteko alisema hatua ya kufuta leseni hiyo ilikuja kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali baada ya Kamati Maalum iliyoundwa kuchunguza biashara ya Madini ya Tanzanite kubaini kuwa leseni hiyo ilitolewa kinyume cha Sheria.
Waziri Biteko aliongeza kuwa, hivi sasa Serikali inaangalia namna bora ya kuligawa eneo hilo kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu ili kuhakikisha kwamba madini ya Tanzanite yanakuwa na manufaa zaidi kwa Taifa na kuchochea ustawi na maendeleo ya nchi kupitia madini hayo na kuongeza kuwa, serikali iliwashirikisha wadau kupata maoni ya namna ya kuligawa eneo husika.
‘’ Serikali nzima inaangalia eneo la Mirerani, eneo hilo linahitaji mazingira rafiki ili wachimbaji wafanye shughuli zao kwa amani na usalama na serikali ipate mapato yanayostahili. Wajibu wetu kama wizara ni kuhakikisha ukuta wa mirerani unapandisha mapato ya serikali,’’ alisisitiza Waziri Biteko.
Pia, aliongeza kuwa, ndoto yake kama Waziri wa Madini ni kuona biashara ya Tanzanite inafanyika ndani ya ukuta katika Kituo cha Pamoja cha Biashara ya Madini ya Tanzanite (One Stop Center) kilichojengwa na serikali na kuongeza kuwa, hata hivyo, serikali haizuii madini hayo kuuzwa katika masoko mengine.
Vilevile, Waziri Biteko alitaka mamlaka zinazohusika na usimamizi wa eneo hilo kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa bila kuvuruga taratibu na kuongeza kuwa, ‘’ Tume ya Madini iliundwa maalum kwa ajili ya usimamizi wa rasilimali madini’’.
Katika hatua nyingine, Waziri Biteko alizitaka Ofisi za Madini nchini kuhakikisha zinatoa ushirikiano kwa taasisi nyingine za serikali katika masuala yanayohusu Sekta ya madini ili kuweka mazingira rahisi ya utekelezaji wa majukumu katika sekta, zikiwemo Kamati za Ulinzi na Usalama katika maeneo husika.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Hussein Mwinyi aliishauri wizara kutoa taarifa kwa wizara hiyo endapo itakuwa na mahitaji maalum ya ulinzi katika eneo hilo na kutumia fursa hiyo kukipongeza kikosi maalum kinachofanya kazi eneo hilo kwamba, kinatekeleza wajibu wake ipasavyo.
“ Mhe. Waziri nafurahi kusikia kwamba, Jeshi Mirerani linatekeleza majukumu yake kikamilifu na hakuna mwingiliano. Endapo mtakuwa na mahitaji maalum mtatutaarifu sisi,’’ alisema Waziri Mwinyi.
Naye, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumza katika kikao hicho, alizitaka taasisi za Serikali zinazozimamia sekta ya madini kuhakikisha zinaelewa na kufahamu matakwa ya Sheria zinazosimamia sekta ya madini.
‘’ Ni vizuri kukumbushana mara kwa mara na ni vizuri wadau wajue kuwa kutokujua sheria siyo tiketi ya kuvunja sheria,’’ alisema Naibu Waziri.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mpaka wa eneo la Kitalu C, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila alisema kuwa mpaka uliowekwa mwaka 1987 ndiyo halali na huo ndiyo msimamo wa Wizara ya Madini. Akizungumzia suala la miundombinu ya TanzaniteOne, alisema kuwa, serikali itaweka utaratibu maalum wa namna ya kushughulikia suala hilo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga alizitaka taasisi za umma kuhakikisha zinazingatia na kutekeleza kwa weledi matakwa ya Sheria ya Tawala za Mikoa ili kuwezesha utekelezaji mzuri wa majukumu ya serikali.
Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Madini Edwin Igenge, alitoa mada kwenye kikao hicho kuhusu Kanuni za Madini (Udhibiti wa Eneo la Mirerani, 2019) kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja katika usimamizi wa shughuli za eneo hilo.
Naye, Mkurugenzi wa Leseni Tume ya Madini Mhandisi Yahaya Samamba alitoa mada kuhusu Historia ya Uchimbaji Madini ya Tanzanite na Changamoto zake, ambapo alieleza kuwa, Tume ya Madini iliifuta Leseni ya Tanzanite mnamo tarehe 23 Desemba, 2019 baada ya kampuni ya TML kuandika barua serikalini Desemba 10 kuomba kuachia eneo hilo na mbia mwenza STAMICO aliridhia ombi hilo Desemba 19, 2019.
Kikao hicho kilijadili masuala mbalimbali yanayohusu shughuli za uchimbaji Madini ya Tanzanite, changamoto na namna ya kuzitatua pamoja na usimamizi wa eneo hilo, kwa lengo la kuboresha shughuli za uchimbaji wa Tanzanite, biashara ya Tanzanite ikiwemo kuhakikisha Serikali inapata mapato stahiki kupitia madini hayo kufuatia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali wa ujenzi wa Ukuta unaozunguka machimbo ya Tanzanite, Mirerani.
Social Plugin