Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba ameiomba serikali kuhakikisha inafunga mipaka haraka kuzuia wageni wanaoingia nchini ambao nchi zao zimekumbwa na maambukizi ya virusi vya corona.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Alhamisi Machi 19, Profesa Lipumba alisema kuendelea kuacha mipaka hiyo bila udhibiti wa wageni hao ni kuendelea kuhatarisha usalama wa afya za wananchi.
Alisema ni vema kukaongezwa uwezo wa vipimo na wataalamu wa kutosha ili kuwabaini wasafiri wanaoingia nchini wanaotoka sehemu mbalimbali za nchi.
“Wakati sasa umefika wa serikali kuamua kufanya uamuzi wa kufunga mipaka yetu, kuweka wataalam na vifaa vya kutosha kwani ugonjwa huu ni hatari na ukiendelea kuingia hapa nchini hali itakuwa mbaya zaidi kwakuwa hata mataifa tajiri wanahangaika nao,”amesema Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba ameongeza kuwa wataalamu wasiishie kupima tu kiasi cha joto bali ni vizuri wakajiridhisha zaidi kwa kuchunguza afya ya wasafiri hao.
Hata hivyo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania (IGP) Simon Sirro amesema jeshi hilo limejipanga imara kwenye mipaka ili kuhakikisha kwamba watu wanaoingia nchini wanafuata utaratibu na endapo wakibainika kuwa na viashiria vya virusi vya Corona basi hatua zinachukuliwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
IGP Sirro amesema kwa sasa hakuna haja ya kufungwa kwa mipaka lakini kama kutakuwa na sababu ya moja kwa moja vyombo vya usalama vilivyopo katika mipaka vitashauri lakini kutokana na Intelijensia walizozipata hakuna tishio kubwa kiasi hicho mpaka kufikia kufungwa mipaka.
"Sasa elimu tumeshaipata kilichobaki ni sisi watanzania kutekeleza hiyo elimu ambayo tumeipata, manaake ukiipata hiyo elimu, usipoitumia hiyo elimu ukabaki kufanya mambo yako ya zamani mwisho wa siku utaangamiza jamii ya Watanzania" Alisema.
Social Plugin