WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AMUAGIZA DC KILINDI KUWACHUKULIA HATUA KALI WANAOUZA ARDHI BILA KIBALI CHA HALMASHAURI


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Kilindi Sauda Mtondoo kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wanaouza ardhi kiholela bila kibali cha Halmashauri kutokana na kwamba wao ndio chanzo cha migogoro ya wakulima na wafugaji.


Majaliwa aliyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi Kata ya Kwediboma wilayani Kilindi mkoani Tanga kwenye mkutano wa hadhara wakati wa ziara yake ya siku sita mkoani hapa ambapo pamoja na mambo mengine alipata fursa ya kusikiliza kero zinazowakabili wananchi na kuzitoa ufafanuzi.


Kauli ya Waziri Mkuu inatokana na miongoni mwa mabango yaliyoonyeshwa kwenye mkutano wake na mmoja wa wananchi wa Kata hiyo akieleza uwepo wa migogoro ya ardhi jambo ambalo lilimlazimu kutoa kauli hiyo


Waziri Mkuu alimtaka Mkuu huyo wa wilaya kuhakikisha wanazipatia ufumbuzi changamoto za migogoro ya ardhi zilizopo kwenye maeneo yao kwani zimekuwa zikikwamisha juhudi kubwa maendeleo kutokana na wananchi kutumia muda mwingi kutafuta  suluhu badala ya kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji. 


“Mkuu wa wilaya hapa Kilindi nimepata malalamiko kwamba kuna migogoro ya ardhi na hili limekuwa ni tatizo kubwa sana hivyo nikuagize kwamba wale wote wanaouza ardhi bila kibali cha Halmashauri wachukuliwe hatua za kisheria”Alisema Waziri Mkuu.


“Kwani wamekuwa wakituingiza kwenye migogoro isiyokuwa ya muhimu na siku ile madiwani wenzangu nimewaambia msijiingize kwenye mambo ya kukata mipaka ipo imeshachorwa na ipo na ramani zipo sasa wewe ukisema mpaka hapo sio sawa”Alisema


Waziri Mkuu alisema kwamba mkoa huo ulikuwa kwenye mkoa kabla ya kugawanya manyara  na Tanga na Arusha kulikuwa na ramani ingawa mikoa haibadiliki ramani ni ileile haiwezekani kubadilishwa mipaka ya kimkoa ipo vile vile.


“Hivyo tunagombania nini hapa sasa…. vongozi tuache tabia ya kuwaingiza wananchi kwenye migogoro isiyokuwa muhimu niliwambia siku ile haizuiliki mwananchi wa Kilindi kwenda kulima Kiteto na wa kiteto kufanya hivyo kilindi lakini zifuatwe taratibu kwa mamlaka husika”Alisema


Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo,Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Anjelina Mabula alisema changamoto kubwa  ya wilaya ya Kilindi ni migogoro mingi ya ardhi kama alivyosema Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella.


Alisema kwamba wao kama wizara wanalitambua hilo na walikwishakutana na wapo kwenye hatua nzuri kuhakikisha migogoro yote inakwisha ili wananchi waweze kuishi kwa amani kwenye maeneo yao.


“Lakini katika jambo hilo suluhu kubwa kuwafanya wana kilindi kuwa na amani ni kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye maeneo yao yote kama tulivyofanya kwenye mkoa wa Morogoro kwenye wilaya ya Kilomober,Ulanga na Malinyi”Alisema


Aidha alisema kwa sababu changamoto iliyopo ni namna ya matumizi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na tatizo kubwa kama alivyoeleza Mkuu wa mkoa ni viongozi kutokuwa waaminifu na watu kutokutambua mipaka yao vizuri.


Hata hivyo alieleza Waziri Mkuu kwamba serikali haijafumbia macho suala hilo na wamelifikisha kwenye hatua nzuri na muda sio mrefu wanakwenda kulipatia suluhu ya moja kwa moja kuachana na migoigoro hiyo.

Waziri Mkuu bado yupo mkoani Tanga kwa ziara ambapo kesho anatarajiwa kuendelea na ziara yake kwenye wilaya ya Lushoto

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post