Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga amesema watamchukulia hatua Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kwa kitendo chake cha kusambaza taarifa za uongo kuhusu mauaji ya watu 14 wilayani Manyoni mkoani Singida.
Lema anadaiwa kutoa taarifa hizo hilo Februari 2020 wakati akizungumza katika mazishi ya katibu wa Chadema jimbo la Singida Mashariki, Alex Joas ambaye mwili wake ulikutwa kando ya barabara ukiwa na majeraha kichwani.
Akizungumza leo Machi 12, 2020, DPP Mganga amesema kuwa taarifa alizozitoa Lema zimeleta taharuki kwa Watanzania na kuwafanya wasiishi kwa amani na kwa jambo hilo lazima atalichukulia hatua na kwamba alichokisema Mbunge Lema ni kauli za kisiasa, kwani matukio hayo yote yalikwishachukuliwa hatua stahiki.
"Na kama yeye aliona hawa wamechinjwa na anawajua waliowachinja kwa mujibu wa sheria yeye anawajibika kutoa taarifa Polisi, Lema naomba ajitokeze aje kuniambia ni lini alienda kutoa taarifa kwamba kuna watu wanachinjwa na hatua hazikuchukuliwa" amesema DPP Biswalo Mganga.
Aidha DPP Mganga ameongeza kuwa "Tunapochukua hatua mnielewe, hatuwezi kuendelea kuwa Taifa la watu wenye uzushi, kwa hili nitachukua hatua, hatuwezi kuendelea kuwa na upotoshaji wa namna hii, halafu watu wanasema wanasiasa wa vyama vya upinzani wanaonewa wakati wanafanya upuuzi".
Social Plugin