Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : MWENYEKITI WA TCDC DK. TITUS KAMANI AZINDUA MNADA WA CHOROKO KWA MFUMO WA MTANDAO SHINYANGA,MWANZA


Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Dk. Titus Kamani akizungumza na Wakulima wa zao la Choroko na wanachama  wa Vyama vya Msingi vya Ushirika wakati akizindua Mnada wa zao la Choroko kwa Mfumo wa Mtandao “Online Trading System”.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (Tanzania Cooperative Development Commission -TCDC ) Dk. Titus Kamani amezindua Rasmi Mnada wa zao la Choroko kwa Mfumo wa Mtandao “Online Trading System” katika Mkoa wa Shinyanga na Mwanza.

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatano Machi 11,2020 katika kijiji cha Manigana kata ya Solwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Dk. Kamani alisema lengo la serikali ni kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao na kuuza mazao yao kwa bei nzuri hivyo anaamini Mnada wa Choroko kwa kutumia mfumo wa mtandaoni utasaidia wakulima kuuza mazao kwa bei ya juu.

“Wakulima mlikuwa mnauza choroko kwa bei ya chini inayoumiza,vitini vya choroko vilikuwa vinachezewa. Na sasa ili kupata bei nzuri ni kwenda mnadani ambapo kutakuwa na bei ya ushindani na ukiridhika na bei ndiyo unauza na kupewa fedha zako”,alisema Dk. Kamani.

“Hamasisheni wakulima wajiunge kwenye Vyama vya Msingi ‘AMCOS’ ,kwani mnada utafanyika kupitia AMCOS ambapo kila mkulima atapeleka choroko yake na kuangalia bei ya ushindani itakayokuwepo siku ya mnada na atalipwa fedha zake ndani ya saa 72”,aliongeza Dk. Kamani.

Aidha alisema mbali na Mnada kwa mfumo wa Mtandao kumnufaisha mkulima pia utasaidia Chama Kikuu Cha Ushirika na Halmashauri za wilaya kupata fedha huku akisisitiza kuwa bei ya ushindani inakwenda kwa mkulima bila makato.

Kwa upande wake, Kaimu Mrajis Msaidizi Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Benjamini Mwangala alisema uzinduzi huo wa Mnada wa zao la Choroko kwa Mfumo wa Mtandao “Online Trading System” ni sehemu ya utekelezaji wa Tangazo la Waziri wa Kilimo alilolitoa Februari 14,2020 kuzindua Mnada wa Soko la Bidhaa kwa mazao ya jamii ya mikunde na mbegu.

“Tangazo hilo linataka mazao ya Jamii ya Mikunde na mbegu kama vile mbaazi,choroko,dengu,ufuta na soya kuuzwa kupitia Vyama vya Ushirika ili mkulima apate bei nzuri na ya ushindani mahali alipo”,alisema Mangwala.

Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Soko la Bidhaa, Augustino Mbulumi alisema katika mnada wa leo Machi 11,2020 jumla ya kilo 2000 za choroko zimeuzwa kwa bei ya shilingi 1340 kwa kilo moja.

Aliwasihi wakulima wajikusanye wapeleke mazao yao katika AMCOS na kukusanya mazao mengi ili kuvutia wanunuzi wakubwa wenye bei nzuri ili mkulima anufaike kupitia zao hilo la choroko.

Naibu Mrajis wa Vyama Vya Ushirika Tanzania, Charles Malunde alisema serikali itahakikisha mazao yote yanaingia katika mfumo wa Stakabadhi ghalani ambapo mnada utakuwa unafanyika kupitia mtandao ili wakulima wanufaike kupitia kilimo.

Mkulima wa choroko Kwiyolecha Nkilijiwa aliiupongeza serikali kwa kuanzisha mnada wa mazao akieleza kuwa wakulima walikuwa wanapata hasara kutokana na kuuza choroko yao kwa bei ya chini ambapo hapakuwa na vipimo walanguzi walikuwa wananunua kwa Rumbesa/visado kuanzia shilingi 600 hadi 1000.

ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Dk. Titus Kamani akizungumza na Wakulima wa zao la Choroko na wanachama  wa Vyama vya Msingi vya Ushirika wakati akizindua Mnada wa zao la Choroko kwa Mfumo wa Mtandao “Online Trading System” katika moja ya Ghala kwenye kijiji cha Manigana kata ya Solwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga leo Jumatano Machi 11,2020. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Dk. Titus Kamani akiwahamasisha wakulima kuuza zao la choroko kwa kutumia mnada kupitia mfumo wa Mtandao ili waweze kuuza choroko kwa bei ya ushindani.
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Dk. Titus Kamani akiwahamasisha wakulima wajiunge kwenye Vyama vya Msingi ‘AMCOS’.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Soko la Bidhaa, Augustino Mbulumi akielezea jinsi Mnada kwa mfumo wa Mtandao 'Online Trading System' unavyofanya kazi na kusaidia kupata wanunuzi kutoka nje ya nchi kwa ushindani.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Soko la Bidhaa, Augustino Mbulumi akionesha matokeo ya mnada wa leo Machi 11,2020 jumla ya kilo 2000 za choroko zimeuzwa kwa bei ya shilingi 1340 kwa kilo moja.
Katika mnada wa leo Machi 11,2020 wanunuzi wawili walijitokeza kununua choroko kiasi cha kilo 2000 ambapo mnunuzi wa kwanza alitoa bei ya shilingi 1340 na mnunuzi wa pili alitoa shilingi 1,248 kwa kilo moja kununua kilo 2000 za choroko.
Naibu Mrajis wa Vyama Vya Ushirika Tanzania, Charles Malunde akizungumza wakati wa uzinduzi Mnada wa zao la Choroko kwa Mfumo wa Mtandao “Online Trading System” ambapo alisema serikali itahakikisha mazao yote yanaingia katika mfumo wa Stakabadhi ghalani ili wakulima wanufaike kupitia kilimo.
Naibu Mrajis wa Vyama Vya Ushirika Tanzania, Charles Malunde akizungumza wakati wa uzinduzi Mnada wa zao la Choroko kwa Mfumo wa Mtandao “Online Trading System” ambapo alisema serikali itahakikisha mazao yote yanaingia katika mfumo wa Stakabadhi ghalani ili wakulima wanufaike kupitia kilimo.
Kaimu Mrajis Msaidizi Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Benjamini Mwangala akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mnada kwa Mfumo wa Mtandao kwa ajili ya zao la Choroko. Alisema uzinduzi huo waMnada wa zao la Choroko kwa Mfumo wa Mtandao “Online Trading System” ni sehemu ya utekelezaji wa Tangazo la Waziri wa Kilimo alilolitoa Februari 14,2020 kuzindua Mnada wa Soko la Bidhaa kwa mazao ya jamii ya mikunde na mbegu.
Wakulima  na  wanachama wa AMCOS wakiwa kwenye uzinduzi wa Mnada wa zao la Choroko kwa Mfumo wa Mtandao “Online Trading System”.
Kushoto ni Naibu Mrajis wa Vyama Vya Ushirika Tanzania, Charles Malunde akifuatiwa na Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU), Ramadhani Kato na Kaimu Mrajis Msaidizi Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Benjamini Mwangala wakiwa kwenye uzinduzi wa Mnada wa zao la Choroko kwa Mfumo wa Mtandao “Online Trading System”.  
Sehemu ya choroko ikiwa kwenye magunia katika ghala la kijiji cha Manigana kata ya Solwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Kushoto ni Mkulima wa choroko Kwiyolecha Nkilijiwa akiteta jambo na Naibu Mrajis wa Vyama Vya Ushirika Tanzania, Charles Malunde wakati wa uzinduzi wa Mnada wa zao la Choroko kwa Mfumo wa Mtandao “Online Trading System”.  
Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Dk. Titus Kamani akipiga picha ya kumbukumbu na viongozi mbalimbali.
Katikati ni Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU), Ramadhani Kato akizungumza na Mkulima wa choroko Kwiyolecha Nkilijiwa. Kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania Dk. Titus Kamani.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com