Mkunga akimbeba mtoto mchanga nchini Zimbabwe
Maafisa wa polisi nchini Uganda wanachunguza kisa kimoja ambapo mkunga mmoja aliripotiwa kumuhudumia visivyo mama mjamzito aliyekuwa katika uchungu wa kujifungua ambapo kichwa cha mwanawe kilikatika.
Inadaiwa kwamba muuguzi huyo alimvuta mtoto huyo kwa kutumia nguvu nyingi mtoto huyo ambaye tayari alikuwa amefariki na kuishia akibeba kiwiliwili chake wakati mama huyo alipokuwa akijifungua.
Wakati mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 21 alipoingia katika chumba cha kujifungua , familia yake inasema kwamba alisubiri kwa muda mrefu kabla ya kuhudumiwa.
Kwa siku nne mfululizo alikuwa amelazwa katika Kituo cha Afya cha Bulumbi 111 akisubiri wakati mwafaka wa kujifungua mwanawe.
Kulingana na gazeti la Daily Monitor , wakati mmoja familia yake iliwasilisha ombi la kuitaka hospitali hiyo kumhamisha hadi katika kituo cha msalaba mwekundu iwapo hospitali hiyo ilikuwa imeshindwa kumsaidia ajifungue.
Kulingana na gazeti hilo babake mtoto huyo alisema: Tulienda hospitalini siku ya Alhamisi, iwapo walikuwa wameona tatizo lolote wangekuwa wangetuhamishia kwenye kituo cha msalaba mwekundu , lakini wakalazimika kutumia nguvu.
Wakati mkunga huyo alipokuwa akimhudumia muda wa saa sita mchana , miguu ya mtoto ilikuwa ya kwanza kutoka lakini mtoto akakwama kuanzia mabegani kwenda juu.
Inasemekana kwamba Mkunga aliyekuwa anamsaidia mama huyo kujifungua alimvuta mtoto huyo na baadaye kwenda kuketi chini. Baadaye alirudi akamvuta mtoto na kuanza kumgeuza geuza. Muuguzi huyo hatahivyo anadaiwa kuomba usaidizi kutoka kwa muuguzi mwenzake.
Muuguzi huyo alimvuta mtoto huyo huku akimgeuzageuza na baadaye mtoto akatoka lakini bila kichwa.
Babake mtoto huyo alisema: Wakati mtoto alipotoka , muuguzi aliendelea kumvuta mtoto na kumrudisha ndani . Mtoto alikufa kifo kibaya .Serikali inahitaji kuwafunza hawa watu.
Bi Musazi anasema kwamba mwanawe alikuwa mzima kutokana na ushahidi wa miguu yake iliokuwa ikicheza.
Kisa hicho kimezua hisia kali nchini Uganda huku wakaazi wakitoa wito kwa serikali kuwafunza wakunga jinsi ya kusaidia katika kujifungua.
Bwana Ibrahim Okelo ambaye ni mwenyekiti wa kijiji hicho alisema: Tunaitaka serikali kuwabadilisha wakunga hao na msimamizi wa hospitali,
Mwili wa mtoto huyo ulipelekwa kituo cha Afya cha Busia kwa uchunguzi kabla ya kupelekwa nyumbani kwa mazishi.
Maafisa wa polisi wamesema kwamba wanachunguza kesi hiyo wanayodai kuwa kisa cha uzembe dhidi ya mkunga huyo.
Wakaazi wanadai kwamba katika kipindi cha miezi mitatau , wanawake wawili na watoto wawili wamefariki wakati wa kujifungua katika kituo hicho.
Maafisa wa polisi wanadaiwa kuwa walipelekwa ili kuweka usalama katika kituo hicho cha Afya baada ya wakaazi kujaribu kukivamia kutokana na masuala hayohayo.
Jaribio la gazeti la Daily Monitor kuzungumza na msimamizi wa kituo hicho cha Bulumbi 111 pamoja na afisa wa afya wilayani hazikufua dafu kwa kuwa hawakushika simu zao.
Wale walioshika simu walisema kwamba hawajaruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari.
CHANZO- BBC