Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UPENDO KASWAGA: MIMI NI MUSAGANE SIJAKEKETWA LAKINI NI KIONGOZI NAONGOZA



Katibu Tarafa ya Inchugu wilaya ya Tarime Upendo Kaswaga akizungumza wakati wa siku ya wanawake duniani wilaya ya Tarime mkoani Mara.


Na Dinna Maningo - Tarime
Katibu Tarafa ya Inchugu wilaya ya Tarime mkoani Mara Upendo Kaswaga amewataka wanawake kutoogopa kuitwa Musagane (Mwanamke ambaye hajakeketwa) badala yake wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Kaswaga aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Nyabitocho Kata ya Mbogi wilayani humo yenye kauli mbiu isemayo kizazi cha usawa kwa maendeleo ya Tanzania ya sasa na baadae, aliwahimiza wanawake kujisimamia.

Kaswaga alisema kuwa wanawake waipuuze misemo ya kimila kwa kuwa ilishazoeleka na haina athari kwa mwanamke na kwamba watumie nafasi hiyo kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi za uongozi.

Alisema kuwa yeye ni Musagane hajakeketewa lakini ni kiongozi anaongoza na jamii inamsikiliza na kwamba anaamini kuwa mwanamke anaweza bila hata kuwezeshwa ilimradi tu anajisimamia vyema.

"Mimi ni musagane sijakeketwa lakini n ikiongozi, ni katibu Tarafa wa Inchugu na siogopi kuitwa musagane kwakuwa hainipi athari yoyote,wanawake wenzangu msiogope jitokezeni kugombea mkiwa kiongozi mtawaongoza na hawatakuwa na ujanja wowote kwakuwa watakuwa chini yenu watawasikiliza hata kama ni musagane maana wewe ni kiongozi", alisema Kaswaga.

Alisema kuwa siku ya wanawake duniani imewekwa ili kuwakumbusha wanawake haki zao ikiwa ni pamoja kuiondoa dhana inayosemwa na wanaume kuwa mwanamke hawezi mpaka awezeshwe.

Kaswaga alipinga vikali kauli ya kwamba mwanamke anaweza akiwezeshwa na kudai kuwa wanawake wamekuwa wakifanya kazi kwa kujisimamia wenyewe bila kusukumwa na wanaume na wamekuwa na maendeleo makubwa.

" Wanaume wanasema sisi tunaweza mpaka wakituwezesha si kweli sisi tunaweza tukijisimamia mama Samia Suluhu ni Makamo wa Rais tunamwona anavyochapa kazi na viongozi wengine ni kwasabu wanajisimamia,akina mama sisi ni mashujaa tunapokuwa kazini tunachapa kazi tukirudi majumbani kwetu tunahudumia familia na maisha yanasonga",alisema Kaswaga.

Aliwataka wanaume kutowanyanyasa wanawake nakwamba wanawake wamechoka vipigo jambo linalosababisha baadhi yao kuzikimbia familia na wanapoondoka watoto uteseka kwakuwa wanaume hawajui kulea watoto kama anavyolea mama. 

Aliwataka wananchi kutowajengea chuki viongozi wanaosimamia haki za mtoto wa kike huku akiyashukuru mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotetea haki za wasichana ikiwa ni pamojana kupinga vitendo vya ukeketaji nakueleza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika kumlinda mtoto wa kike.

Kaimu Afisa Elimu msingi wilaya ya Tarime Marina Ngailo aliwataka wanawake kushirikiana kuhakikisha mtoto wa kike tangu akipozaliwa hadi kufika elimu ya juu anapata malezi bora yenye usawa na mtoto wa kiume.

Ngailo alisisitiza mgawanyo wa majukumu katika ngazi za familia" Watoto wa kike wanafanya kazi nyingi wanapokuwa nyumbani jambo linalowasababisha kuchelewa shuleni au kutofanya vuzuri katika masomo yao,hata mtoto wa kiume afanye kazi za nyumbani kushirikiana na mtoto wa kike siyo mtoto wakike abaki nyumbani kulea watoto wakiume yeye anaenda shule",alisema Ngailo.

Afisa utumishi Halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye ni mlemavu wa viungo Pamela Antony alisema kuwa ofisi ya utumishi imekuwa ikizingatia usawa kwa kuajili wanawake na wengine kupewa nafasi za juu za uongozi.

Alisema kuwa halmashauri ina wakuu wa idara wanawake nakwamba wanawake wakiwa na kazi watasomesha watoto na kuchangia maendeleo mbalimbali huku akiwataka wanaume kuwapa nafasi wanawake kuchangia mawazo yao kwenye familia bila ubaguzi.

Akisoma Risala kwa mgeni rasmi Elizabeth Sangija ambaye ni katibu wa vikao halmashauri ya wilaya ya Tarime kuwa halmashauri imekuwa ikitoa mikopo asilimia 10 kuwawezesha wanawake,Vijana na Wamemavu ili kujiinua kiuchumi kujikomboa na umaskini.

Sangija alisema kuwa  katika mwaka 2015-2020 Halmashauri imetoa mkopo kwa wananchi wenye thamani ya Bilioni moja na milioni 622 kwa vikundi 441,na kati ya vikundi hivyo, vikundi 264 ni vya wanawake vyenye wajumbe 3,973 mkopo uliogharimu sh.milioni 987 na laki 5 fedha ambazo ni mapato ya ndani ya halmashauri.

Alimpongeza Rais John Magufuli kwa kuonyesha nia ya dhati katika usawa wa kijinsia kwa kuteuwa wanawake kusimamia katika nafasi mbalimbali za uongozi. 

Katika sherehe hizo wanaume nao hawakuwa nyuma katika kutetea haki za wanawake ambapo Diwani wa kata ya Mbogi Ezekiel Matiko alimtaka Mkurugezi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Apoo Tindwa kupeleka mwalimu wa kike shule ya Sekondari ya Mbogi ambayo haina mwalimu mwanamke huku akiomba Zahanati isajiliwe kuwawezesha wanawake wakiwemo wajawazito kupata huduma ambao wakati wa kujifungua ulazimika kubebwa kwenye machela kwenda kupata huduma ya afya kijiji cha Gitenga 

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Apoo Tindwa alitoa rai kwa wanaume kutowanyanyasa wanawake badala yake watambue umuhimu wa mwanamke katika familia huku Afisa kilimo wa halmashauri hiyo Sylvanus Gwiboha akieleza kuwa wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika shughuli za kilimo kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali jambo ambalo limesaidia kutokuwepo kwa tatizo la njaa.

Pili Elizabeth Sangija akisoma risala siku ya mwanamke duniani iliyofanika kiwilaya kijiji cha Nyabitocho

Wanawake wa Tarime wakisherekea siku ya wanawake duniani

Kaimu afisa elimu msingi wilaya ya Tarime akicheza siku ya maadhimisho ya wanawake duniani

Afisa Utumishi halmashauri ya wilaya ya Tarime ambaye pia ni mlemavu wa viungo Pamela Antony akizungumza wakati wa kushereka siku ya wanawake duniani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com