Na Munir Shemweta, WANMM UKEREWE
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameagiza kufanyika utambuzi wa mipaka sambamba na kuweka alama katika eneo lenye mgogoro wa ardhi kati ya Kanisa Katoliki, wananchi na shule ya msingi ya Kagunguli iliyopo wilaya ya Ukerewe mkoa wa Mwanza.
Uamuzi huo unafuatia kuibuka mgogoro kati ya Mapadri wa Kanisa Katoliki na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cornel Magembe kuhusu umiliki wa sehemu ya eneo la shule ya msingi Kagunguli jambo lililosababisha Mapadri kuandika waraka wa kutoshirikiana na mkuu huyo wa wilaya.
Akizungumza katika kikao cha utatuzi wa mgogoro huo uliohusisha Mapadri, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Serikali ya Kijiji jana wilayani Ukerewe mkoani Mwanza Dkt Mabula alisema maamuzi yote yaliyotolewa nje ya utaratibu kuhusiana na mgogoro huo ni batili na usubiriwe utambuzi wa mipaka ya eneo lenye mgogoro.
‘’ Wizara itatuma timu ya wataalamu ili kutafuta ufumbuzi wa mgogoro kwa kubainisha na kutambua mipaka ya hapa eneo Kagunguli na kuja na ufumbuzi wa kudumu’’ alisema Dkt Mabula.
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameagiza kupatiwa barua za maeneo yote ya taasisi za dini yenye migogoro mikubwa ya ardhi ili iweze kushughulikiwa na kubainisha kuwa katika kuishughulikia migogoro hiyo timu ya wataalamu itatumwa katika maeneo husika kwa lengo la kubainisha uhalali wa pande zenye migogoro.
Alimtaka Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ukerewe Estar Chaula kujiandaa kugharamia wataalamu watakaokwenda kubainisha mipaka yenye mgogoro katika halmashauri yake kwa kuwa halmashauri ndizo zenye jukumu la kupanga maeneo yake.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema kitakachofanywa na wizara yake sasa kuhusiana na mgogoro huo ni kwenda kufufua mipaka na kuanisha matumizi ya eneo hilo ambapo alisisitiza kuwa ni vizuri maeneo yote ya umma yakawekewa mipaka yenye alama zinazoonekana.
Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cornel Magembe aliweka wazi kuwa, mgogoro uliopo katika eneo linalohusisha shule ya Sekondari Kagunguli inayomilikiwa na Kanisa Katoliki umechochewa kwa kiasi kikubwa na Mkuu wa shule ya Sekondari Kagunguli Padri Johanes Nawachi kwa kile anachodai padre huyo eneo la shule yake kuvamiwa.
Hata hivyo, Magembe alisema katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo aliagiza Kanisa Katoliki kuwasilisha Hati ya umiliki eneo lake, huku serikali ya kijiji nayo ikitakiwa kuwasilisha muhtasari wa kijiji kuhusiana na kutolewa sehemu ya eneo sambamba na nyumba tatu za walimu wa shule ya msingi Kagunguli kubaki kama zilivyo ndipo afanye maamuzi kuhusiana na mgogoro huo.
Alisema, kilichofanywa na Mapadri wa Kanisa Katoliki kuandika waraka wa kutoshirikiana naye ni uchochezi kwa waumini wa kanisa hilo na serikali na kubainisha kuwa hali hiyo imesababishwa na msimamo wake wa kuhakikisha maeneo ya serikali yanalindwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kagunguli Padri Johanes Nawachi alisema kumekuwa na mahusiano mabaya baina yake na Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cornel Magembe baada ya kuanza zoezi la kupanda miti eneo alilodai kumilikiwa na kanisa Katoliki na kuhusisha pia maeneo ya nyumba tatu za walimu wa shule ya msingi Kagunguli.
Social Plugin