Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NHC YATAKIWA KUKAMILISHA UJENZI JENGO LA KITEGA UCHUMI MUTUKULA

Na Munir Shemweta, WANMM MISENYI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi DkT Angeline Mabula amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kukamilisha haraka mradi wake wa ujenzi wa Jengo la Kitega Uchumi lililopo mpaka wa Tanzania na Uganda eneo la Mutukula wilaya ya Misenyi mkoani Kagera ili kuliwezesha shirika kupata faida kupitia jengo hilo.

Dkt Mabula alitoa agizo hilo juzi wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo akiwa katika ziara yake mkoani Kagera kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo sambamba na kufuatilia utekelezaji maagizo aliyoyatoa kuhusiana na wa sekta ya ardhi.

Alisema, mradi wa jengo la kitega uchumi unaoendelea eneo la Mutukula uko sehemu nzuri ya mpakani mwa Tanzania na Uganda na kuna muingiliano mkubwa wa kibiashara hivyo ni vizuri Shirika la Nyumba likaona haja ya kuharakisha ujenzi wake ili kutoa fursa kwa taasisi na wawekezaji kupanga kwenye jengo hilo.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, mji wa Mutukula umechangamka na una mzunguko mzuri wa biashara hatua inayosababisha kuwepo mvuto kwa wafanyabiashara na wawekezaji katika eneo hilo na kukamilika kwake kutaiwezesha NHC   kupata wapangaji na kujipatia mapato.

‘’Naagiza Miradi yote ya Shirika la Nyumba la Taifa inayoweza kuliingizia Shirika mapato likiwemo hili la kimkakati lazima iishe ili NHC iingize mapato na kujiendesha kibiashara’’ alisema Dkt Mabula

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mikoa ya Kagera na Geita Benit Masika alisema shirika lake liko katika jitihada kubwa za kuhakikisha mradi huo wa jengo la kitega uchumi Mtukula unakamilika mapema na kubainisha kuwa kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 88 na utakapokamilika litapangishwa kwa taasisi zilizoonesha nia ya kupanga zikiwemo za kifedha kama vile mabenki.

Aidha, Nabu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliitaka halmashauri ya wilaya ya Misenyi mkoani Kagera kutumia vizuri fursa ya kuwa eneo la mpakani kwa kuhakikisha inakamilisha zoezi la kupanga, kupima na kumilikisha viwanja ili wananchi waweze kujenga nyumba nzuri na zenye sura ya nchi ya Tanzania.

Alisema, halmashauri ya Misenyi wakati wa kupanga mji huo ihakikishe inakuwa na soko la mazao zikiwemo ndizi ili kuwawezesha watanzania kuuza bidhaa zao nchini Uganda tofauti na sasa ambapo tegemeo kubwa lipo upande wa Uganda na kuwataka watanzania kubadilika kwa kuitumia fursa ya kuwa eneo la mpakani kuchangamkia kuwekeza katika ardhi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com